AMKA NA BWANA LEO 5

``JUMATATU, JULAI 5, 2021

KESHA LA ASUBUHI, LESONI NA USOMAJI WA BIBLIA KWA MPANGO

KESHA LA ASUBUHI

Jumatatu, Julai 5, 2021

😍SOMO: UKWELI UTASHINDA

Lakini tumekataa mambo ya aibu yaliyositirika, wala hatuenendi kwa hila, wala kulichanganya neno la Mungu na uongo; bali kwa kuidhihirisha iliyo kweli twajionyesha kuwa na haki, dhamiri za watu zikitushuhudia mbele za Mungu. 2 Wakorintho 4:2.

Hakupaswi kuwapo kudhoofisha kweli za msingi ambazo Bwana ameziwasilisha kwa ushahidi mwingi wa kimiujiza. Sauti inapaswa kusikika kwa uthibitisho wa wazi wa ukweli, kinyume na mashaka na uongo ambao umekuwa ukija kutoka kwa adui wa ukweli. Matengenezo yatafanyika, na utendaji wa kanuni za ukweli mtakatifu utadhihirisha ukuaji katika neema, kwani nguvu za Mungu zina ufanisi katika kuelimisha na kutakasa ufahamu wa mwanadamu.

Ukweli kama ulivyo katika Yesu, kama ulivyotangazwa Naye wakati alipofunikwa na wingu kama mawimbi, ni hakika na kweli katika siku zetu hizi, na kwa hakika utarekebisha akili ya mpokeaji kama vile ulivyorekebisha akili siku zilizopita. Kristo ametangaza, "wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa, hata mtu akifufuka katika wafu" (Luka 16:31)

Kama jamii ya watu, lazima tutayarishe njia ya Bwana, chini ya uongozi wenye kutangua wa Roho Mtakatifu, kwa ajili ya kuenea kwa injili katika usafi wake. Kijito cha maji ya uzima kinapaswa kuongezeka kina na kupanuka katika njia yake. Katika nyanja zote, karibu na mbali, watu wataitwa kuacha majembe ya kukokotwa na ng'ombe na kuacha kazi za biashara  ya kawaida ambazo kwa sehemu kubwa hujaza akili, na wataelimika kwa kuunganika na watu ambao wamekuwa na uzoefu watu ambao wanaujua ukweli. Kupitia utendaji wa ajabu wa Mungu, milima ya shida itaondolewa na kutupwa baharini....

Wale wanouhubiri ukweli watajitahidi kuudhihirisha ukweli kwa maisha manyofu na mazungumzo yenye kicho kwa Mungu. Na wanapofanya hivi, watakuwa na nguvu katika kuutetea ukweli na katika kuupatia matumizi ya hakika ambayo Mungu ameupa....

Wito ni kusonga mbele, "Mwanangu, nenda ukafanye kazi leo katika shamba langu la mizabibu." Wito huu unapotiiwa, ujumbe ambao una maana sana kwa wakazi wa dunia, utasikika na kueleweka. Watu watajua kilicho kweli. Mbele, na mbele zaidi, kazi itaendelea. Na matukio dhahiri ya majaliwa ya Mungu yataonekana na kutambuliwa, katika hukumu na katika baraka. Ukweli utanyakua  ushindi

LESONI, JULAI 5

SOMO: UNAAMBUKIZWA

Soma Hesabu 12:1—3. Miriamu na Haruni wamekasirishwa na nini?

Kwa mwonekano wa juu juu, Miriamu na Haruni hawakufurahishwa na mke wa Musa Mkushi. Sipora hakuwa wa jamii ya Israeli akitokea Midiani (tazama Kut. 3:1). Hata miongoni mwa “watu walio bora kabisa” wa Israeli hali ya asili yetu kuanguka inadhihirishwa, na wala si kwa namna ya kupendeza. (ni hakika?) 

Fungu hilo la Biblia, hata hivyo, kwa wazi linaonesha hili kuwa udhuru wa kuficha ukweli. Kiini kikubwa cha manung’uniko yao ni kuhusu kipawa cha unabii. Katika sura iliyotangulia Mungu alimwambia Musa kuchagua wazee sabini wa Israeli ambao wangemsaidia Musa kubeba mzigo wa utawala wa uongozi (Hes. 11:16, 17, 24, 25). Haruni na Miriamu walikuwa na majukumu ya msingi katika uongozi, vile vile (Kut. 4:13—15, Mik. 6:4), lakini sasa wanahisi kutishiwa na uundwaji wa uongozi mpya na kusema, " 'Je, Ni kweli Bwana amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia?' " (Hes. 12:2). 

Mungu anajibuje malalamiko haya? Soma Hesabu 2:4—13. Kwa nini unafikiri Mungu alijibu kwa uthabiti?

Jibu la Mungu ni la mara moja na halihitaji ufafanuzi. Kipawa cha unabii sio silaha ya kujiongezea madaraka zaidi. Musa alikuwa anafaa zaidi kwa uongozi kwa sababu alikuwa amejifunza namna alivyokuwa tegemezi zaidi kwa Mungu. 

Ukweli kwamba Miriamu anatajwa kabla ya Haruni katika fungu la 1 huashiria kwamba yaweza kuwa yeye ndiye aliyekuwa mchochezi wa shambulio kwa Musa. Kwa wakati huu, Haruni tayari alikuwa anahudumu kama kuhani mkuu wa Israeli. Ikiwa angepigwa kwa ukoma, asingeweza kuingia katika patakatifu na kuhudumu kwa niaba ya watu. 

Adhabu ya Mungu kwa Miriamu kwa ukoma wa muda hueleza waziwazi kutokupendezwa kwake na wao wote na husaidia kuleta badiliko la mtazamo ambao familia hii iliuhitaji. Ombi la Haruni kwa ajili yake huthibitisha kwamba yeye, pia, alihusika (Hes. 12:11), na sasa badala ya ukosoaji na kukosa utulivu, tunamwona Haruni akiomba kwa ajili ya Miriamu, na tunamwona Musa anaomba kwa niaba yake (Hes. 12:11—13). Huu ndio mtazamo ambao Mungu anataka kuuona kwa watu wake. Anasikia, na kumponya Miriamu.

Japo ni rahisi mara zote kukosoa uongozi wa kanisa, katika ngazi yoyote, kanisa letu na maisha yetu ya kiroho yangekuwaje bora zaidi ikiwa, badala ya kunung’unika, tungeomba kwa niaba ya viongozi wetu hata wakati tunapotofautiana nao?

Usomaji wa Biblia kwa mpango

LUKA 23

1. Wakasimama mkutano wote, wakampeleka kwa Pilato. 

2. Wakaanza kumshitaki, wakisema, Tumemwona huyu akipotosha taifa letu, na kuwazuia watu wasimpe Kaisari kodi, akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, mfalme. 

3. Pilato akamwuliza, akisema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu akamwambia, Wewe wasema. 

4. Pilato akawaambia wakuu wa makuhani na makutano, Sioni neno lililo ovu katika mtu huyu. 

5. Nao walikaza sana, wakisema, Huwataharakisha watu, akifundisha katika Uyahudi yote, tokea Galilaya mpaka huku. 

6. Pilato aliposikia hayo aliuliza kama huyu ni mtu wa Galilaya. 

7. Na alipopata habari ya kuwa yu chini ya mamlaka ya Herode, alimpeleka kwa Herode, kwa kuwa yeye naye alikuwapo Yerusalemu siku zile. 

8. Na Herode alipomwona Yesu alifurahi sana, kwa sababu alikuwa akitaka sana kumwona tangu siku nyingi, maana amesikia habari zake, akataraji kuona ishara iliyofanywa na yeye. 

9. Akamwuliza maneno mengi, yeye asimjibu lo lote. 

10. Wakuu wa makuhani na waandishi wakasimama wakamshitaki kwa nguvu sana. 

11. Basi Herode akamfanya duni, pamoja na askari zake, akamdhihaki, na kumvika mavazi mazuri; kisha akamrudisha kwa Pilato. 

12. Basi siku ile ile Herode na Pilato walipatana kwa urafiki kwa maana hapo kwanza walikuwa na uadui wao kwa wao. 

13. Na Pilato akawakutanisha wakuu wa makuhani, na wakubwa, na watu, 

14. akawaambia, Mtu huyu mmemleta kwangu kana kwamba anapotosha watu; nami, tazama, nimeamua mambo yake mbele yenu, ila sikuona kwake kosa lo lote katika mambo hayo mliyomshitaki; 

15. wala hata Herode, kwa maana amemrudisha kwetu; basi tazama, hakuna neno lo lote alilolitenda lipasalo kufa. 

16. Kwa hiyo nitamrudi, kisha nitamfungua. [ 

17. Maana ilimlazimu kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa sikukuu.] 

18. Wakapiga kelele wote pamoja, wakisema, Mwondoe huyu, utufungulie Baraba. 

19. Naye ni mtu aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina iliyotokea mjini, na kwa uuaji 

20. Basi Pilato alisema nao mara ya pili, kwa vile alivyotaka kumfungua Yesu. 

21. Lakini wakapiga kelele, wakisema, Msulibishe. Msulibishe. 

22. Akawaambia mara ya tatu, Kwa sababu gani? Huyu ametenda uovu gani? Sikuona kwake hata neno lipasalo kufa. Basi nikiisha kumrudi nitamfungua. 

23. Lakini wakatoa sauti zao kwa nguvu sana, wakitaka asulibiwe. Sauti zao zikashinda. 

24. Pilato akahukumu kwamba haja yao ifanyike. 

25. Akamfungua yule aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina na uuaji, yule waliyemtaka, akamtoa Yesu wamfanyie watakavyo. 

26. Na walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka shamba, wakamtwika msalaba, auchukue nyuma yake Yesu. 

27. Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea. 

28. Yesu akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu. 

29. Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha. 

30. Ndipo watakapoanza kuiambia milima, Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni. 

31. Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu? 

32. Wakapelekwa na wawili wengine, wahalifu, wauawe pamoja naye. 

33. Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto. 

34. Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura. 

35. Watu wakasimama wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake. 

36. Wale askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki, 

37. huku wakisema, Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe. 

38. Na juu yake palikuwa na anwani; HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI. 

39. Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi. 

40. Lakini yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? 

41. Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa. 

42. Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. 

43. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi. 

44. Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, 

45. jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati. 

46. Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu. 

47. Alipokwisha kusema hayo alikata roho. Yule akida alipoona yaliyotukia, alimtukuza Mungu, akisema, Hakika yake, mtu huyu alikuwa mwenye haki. 

48. Na makutano yote ya watu waliokuwa wamekutanika kutazama mambo hayo, walipoona yaliyotendeka, wakaenda zao kwao, wakijipiga-piga vifua. 

49. Na wote waliojuana naye, na wale wanawake walioandamana naye toka Galilaya, wakasimama kwa mbali, wakitazama mambo hayo. 

50. Na tazama, akatoka mtu mmoja, jina lake Yusufu, ambaye ni mtu wa baraza, mtu mwema, mwenye haki; 

51. (wala hakulikubali shauri na tendo lao), naye ni mtu wa Arimathaya, mji mmoja wa Wayahudi, tena anautazamia ufalme wa Mungu; 

52. mtu huyo alikwenda kwa Pilato, akataka kupewa mwili wa Yesu. 

53. Akaushusha, akauzinga sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililochongwa mwambani, ambalo hajalazwa mtu bado ndani yake. 

54. Na siku ile ilikuwa siku ya Maandalio, na sabato ikaanza kuingia. 

55. Na wale wanawake waliokuja naye toka Galilaya walifuata, wakaliona kaburi, na jinsi mwili wake ulivyowekwa. 

56. Wakarudi, wakafanya tayari manukato na marhamu. Na siku ya sabato walistarehe kama ilivyoamriwa.

MUNGU AKUBARIKI SANA```

No comments