TUTAONGEZA UZALISHAJI WA MBEGU ZA ALIZETI-BASHE

Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema Bajeti ya Sekta ya Kilimo kwenye eneo la uzalishaji wa mbegu bora za alizeti imeongezeka mara dufu ili kuongeza uzalishaji wa alizeti kama njia moja wapo ya kupunguza uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi ambapo taifa hutumia kiasi cha nusu tilioni kuagiza bidhaa hiyo.

Naibu Waziri Bashe amesema kwa sasa uzalishaji wa zao la alizeti upo chini na ndiyo maana viwanda vya mafuta ya kula vinalazimika kuzalisha kwa miezi sita badala ya mwaka mzima kutokana na uhaba wa mbegu za mafuta ya alizeti.

Hata hivyo Naibu Waziri Bashe amesema hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa katika kukabiliana na hali hiyo ikiwemo kuitambulisha mbegu mpya ya alizeti aina ya ‘Records’ inayozalishwa na Wakala wa Mbegu nchini (ASA) ambayo imeonyesha kuwa na matokeo mazuri kwa Wakulima.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea kiwanda cha kuzalisha mafuta ya alizeti cha Pyxus Agriculture Tanzania kilichopo jijini Dodoma Naibu Waziri Bashe amesema nchi yetu ina upungufu wa Tani 400,000 za mafuta, ambazo tunahitaji tupate mbegu bora ili tuweze kukidhi mahitaji hayo.

Amesema Serikali imekuwa ikitumia fedha takribani bilioni 470 kuagiza mafuta ambapo alisema wangekuwa na mbegu bora wangeweza kuzalisha na kuiepusha serikali kuagiza mafuta kula nje ya nchi.

“Serikali tumeamua kushirikiana na viwanda kwa ajili ya kutafuta mbegu bora za mafuta ya alizeti, tutawatumia wakala wa mbegu nchini ASA; Lakini pia tutaingalia mbegu ya ‘Records’ ambayo Wakulima wanasema inaonyesha kuwa na matokeo mazuri.” Alisema Bashe.

Amesema kiuhalisia kiwanda cha Pyxus kinahitaji tani 20,000 lakini kwa sasa wanapata tani 10,000 ambazo hazitoshelezi na kuongeza kuwa endapo wangepata kiasi halisi wanachohitaji ingesaidia kutatua tatizo la mafuta ambalo limekuwa kero kwa wananchi.

Amesema Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa uzalishaji mafuta hapa nchini, wanakwenda kutatua changamoto ya uzalishaji wa mafuta ya kula nchini, huku akisema kuwa wanahitaji kupata mbegu za kuingia kiwandani zaidi ya tani milioni 1.3 kwa viwanda vinavyozalisha mafuta ya kula.

No comments