LUCAS AYO ASEMA UZALISHAJI WA PARETO WAONGEZEKA

Mkurugenzi wa Bodi ya Pareto nchini Lucas Ayo (pichani kulia) amesema uzalishaji wa zao la pareto umeongezeka toka tani 2,011 mwaka 2015/16 hadi kufikia tani 2,510 mwaka 2019/20 kati ya lengo la kuzalisha tani 3,000.

Aidha amebainisha kuwa tija imeongezeka toka wastani wa kilo 250 kwa ekari mwaka 2015/16 hadi kufikia kilo 270 kwa ekari mwaka 2019/20 huku wastani wa bei ya chini anayolipwa mkulima imepanda toka shilingi 1500 mwaka 2015/16 hadi shilingi 2,400 mwaka 2019/20 na shilingi 2,500 mwaka 2020/21 kwa kilo moja ya pareto.

Ayo ametaja mkakati wa Bodi ya Pareto katika mwaka 2021/22 ni kuongeza utafiti wa kina kuhusu matumizi mbalimbali ya bidhaa za pareto ikiwemo visumbufu vya mimea mashambani, majumbani na kwenye maghala ya mazao hatua itakayochochea kukuza kilimo na tija cha zao la pareto.


No comments