RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Serikali ya Ujerumani kwa utayari wake wa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza miradi ya maendeleo iliyopangwa na Serikali ya Awamu ya Nane.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo Jana Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Bi Regine Hess.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi Hess kuwa azma ya Serikali ya Ujerumani ya kuendelea kuisaida Zanzibar katika kuendeleza miradi ya maendeleo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuyafikia malengo yaliyowekwa.
Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pia, inathamini sana mashirikiano yaliopo kati yake na Serikali ya Ujerumani na hatua yake ya kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta ya afya ambayo itandelea kuletea manufaa makubwa kwa wananchi wa Zanzibar.
Alisema kuwa azma ya Serikali ya Ujerumani ya kusaidia uendelezaji wa mradi wa maji safi na salama pamoja na mitaro ya maji taka katika eneo la Mji Mkongwe itasaidia katika kuuweka mji huo katika hadhi yake inayotajika sambamba na kuwapelekea wananchi kupata huduma hizo ipasavyo.
Alifahamisha kuwa Serikali ya Ujerumani kwa muda mrefu imekuwa ikiisaidia Zanzibar katika kuimarisha na kuendeleza sekta ya afya hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuzisaidia hospitali ya Abdalla Mzee Pemba na Hospitali ya Kijeshi ya Bububu.
Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba mbali ya Zanzibar kusaidiwa katika kuendeleza miradi katika sekta ya afya ni vyema ikasaidiwa katika uendelezaji miundombinu na mifumo ya afya pamoja na uendelezaji wa rasilimali watu ili kuwe na tija endelevu ya misaada inayotolewa.
0 Comments