JAFO ASISITIZA UFANISI KWA WASHAURI UELEKEZI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo, amewataka washauri elekezi wa Mazingira kufanya kazi zao kwa ufanisi na kwa kufata Sheria ya Mazingira.

Jafo ametoa wito huo leo Juni 11, 2021 katika mkutano wa Wataalamu Elekezi wa Mazingira Tanzania uliofanyika mkoani Dar es Salaam.

Alisema wataalamu wa mazingira wana kazi kubwa ya kuhakikisha mazingira yanakuwa salama.

"Kama tunavyofahamu ajenda kubwa ya Taifa ni kuvutia wawekezaji lakini katika uwekezaji huo kama wataalamu hawatafanya kazi zao kisanifu basi uwekezaji huo utasuasua na kupelekea athari kubwa katika taifa letu upande wa mazingira," alisema.

Aidha Jafo aliwataka wataalamu hao kuwa kinara katika kutoa ushauri wa mazingira kwa wawekezaji ili tuwe na uwekezaji wenye tija na manufaa katika jamii yetu.

Aliongeza kuwa lengo kubwa la mkutano huu ni kujengea uwezo na kupitishana katika kanuni mpya iliyoundwa ya washauri elekezi, lakini pia kupitia mfumo wa namna ya kusajili miradi kwa mtandao, hivyo kupitia mkutano huu wataalam wa mazingira watakuwa mahiri katika utendaji wao

“Napenda niwaambie wawekezaji kuwa suala la kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) ni jambo muhimu sana hii ni kwaajili ya manufaa ya muwekezaji pamoja na Mazingira yetu," alisema.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Samuel Gwamaka alisema hapo awali kulikuwa na kanuni za wataalamu elekezi wa mazingira za mwaka 2005 ambazo zimefutwa kwa sasa na kuundwa kanuni mpya ambazo zilianza rasmi kutumika Machi 19, 2021.

Dkt. Gwamaka hivyo kutokana na majukumu ya Baraza tumetumia fursa hii kushirikiana na Chama cha Wataalamu wa Mazingira Tanzania (TEEA) kuweza kupeana ushauri na maelekezo ili kuweza kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa weledi na kwa mujibu wa sheria.

No comments