FEDHA KUTOKA BENKI YA DUNIA KUSIMAMIWA NA UMMY

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Ummy Mwalimu ameahidi kuhakikisha fedha zinazotolewa na Benki ya dunia zinatumika kwa madhumini yaliyolengwa husuasani, ujenzi wa madarasa yenye ubora katika shule za msingi na Sekondari, ujenzi wa matundu ya vyoo, ujenzi wa maabara na mabweni.

Ameyasema hayo leo jijini Dodoma kwenye kikao cha pamoja na Waziri wa elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Joyce Ndalichako na Mkurugenzi Mtendaji wa wa Benki ya Dunia anayeshughulikia masuala ya Afrika Dkt. Taufila Nyamadzabo kilichojadili utekelezaji wa miradi ya elimu nchini Tanzania

Waziri Ummy ameishukuru benki ya Dunia kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha wanaimarisha ujenzi wa miundombinu katika shule za Msingi na Sekondari Nchini ambapo wameweza kusaidia kutatua changamoto za uhaba wa madarasa , matundu ya vyoo, maabara na maktaba nchini.

Amewakikishia Benki ya Dunia kuwa Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha watoto waliokosa elimu kwa changamoto mbalimbali nao wanapata fursa ya kuendelea na elimu ambapo katika uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano wanafunzi 280 walichaguliwa kujiunga na kidato cha tano kupitia elimu mbadala ya Taasisi ya Elimu ya watu wazima.

Waziri Ummy ameishukuru benki ya Dunia kwa kufuatilia na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya Elimu nchini ili kuhakikisha fedha zilizotolewa zinatekeleza miradi iliyopangwa na kutatua changamoto za elimu nchini.

Aidha amewaagiza wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanajiepusha na kutoa matamko kinzani na msimamo au sera za Serikali , maelekezo ya Serikali katika masuala ya Elimu, wazingatie maelekezo kutoka Serikalini katika utendaji wa kazi zao kwa kuwa kuna masuala mengine yaatakiwa kuamuliwa katika ngazi ya Wizara.

No comments