CHF KUFIKIA ASILIMIA 10 YA WANUFAIKA

Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imejipanga kuendelea kuboresha huduma za CHF ILIYOBORESHWA kwa kuongeza wanufaika wa huduma za afya kutoka asilimia 5 ya mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 10 mwaka 2022.

Hayo yamesemwa na Ziada Nkinda Shekalaghe kwa niaba ya Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais- TAMISEMI wakati akifungua semina ya siku moja kwa waratibu wa mikoa, maafisa habari wa mikoa na maafisa TEHAMA mkoani Mbeya.

"Tumeona umuhimu wa maafisa habari katika kutangaza CHF ILIYOBORESHWA kwani hata mratibu akifanya vizuri bila kuyaandika hayo mazuri hayawezi kufika kwa walengwa ndio maana tumeona umuhimu wenu na tunaamini mtaitangaza CHF ili iwafikie watunwengi zaidi," amesema Bi. Shekalaghe

Aidha amesema hadi kufikia April 2021 jumla ya watu milioni 3 wamejiunga na kufanikiwa kukusanya shilingi bilioni 18 ambapo jumla ya shilingi bilioni 7 zimerudishwa katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya kuboresha huduma za afya.

"Uwepo wenu wote hapa nina imani tutaweza kuboresha zaidi mfuko huu na kufikia asilimia 30 badala ya 10 tuliyojiwekea mwaka 2022 na kufikia lengo la Serikali la bima ya afya kwa wote,"amesisitiza Bi. Shekalaghe

Hatahivyo aliwashauri waratibu wa CHF ILIYOBORESHWA ngazi ya mikoa kutokujifungia peke yao badala yake washirikiane na wengine na kuwaambia kuwa kila mtu kwa nafasi yake anaweza kuinua CHF ILIYOBORESHWA sehemu alipo.

Semina ya siku moja ya CHF ILIYOBORESHWA inafanyika mkoani Mbeya ambapo imehudhuriwa na viongozi kutoka OR TAMISEMI, maafisa Habari wa mikoa, waratibu wa CHF mikoa na Maafisa TEHAMA wa mikoa lengo likiwa kuweka mikakati ya pamoja ya uhamasishaji Jamii kujiunga na CHF iliyoboreshwa kutoka asilimia 6 hadi 10 mwaka 2022 ambapo lengo la taifa ni kufikia asilimia 30 mwaka 2025. 

No comments