BILIONI 24 YATENGWA KUSAMBAZA UMEME VIJIJINI

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, amesema Serikali imetenga shilingi Bilioni 34 zitakazotumika katika Mradi wa kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu mzunguko wa Pili kwa Vijiji 166 ambavyo bado havijafikiwa na Umeme katika Mkoa wa Kagera.

Wakili Byabato, alisema hayo wakati akizindua rasmi mradi huo katika Kijiji cha Omurunazi Wilayani Muleba mkoani humo, uliofanyika Juni 19, 2021.

Alisema kuwa katika kuhakikisha kuwa vijijini vyote vinaunganishwa na Umeme nchini, Mkoa wa Kagera umetengewa fedha hizo ambazo zitatumika katika mradi wa kusambaza umeme kwenye vijiji vyote vilivyosalia katika wilaya Saba za mkoa huo ambao unaotekelezwa kwa kipindi cha miezi 18.

Alifafanua kuwa, kwa Wilaya ya Muleba, ambapo mradi huo umezinduliwa, serikali imetenga shilingi Bilioni 6 ambazo zitatumika kusambaza Umeme katika Vijiji 30, ambapo pia Mkandarasi ametakiwa kuwaunganishia Umeme wateja 400 kwa kuanzia.

“Azma ya Serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwakani 2022, vijiji vyote nchini viwe vimeungamishiwa Umeme, hivyo imetoa muongozo kuwa gharama za kuunganisha Umeme mdogo kuwa ni shilingi 27,000 na kwa Umeme mkubwa ni shilingi 139, 500 kwa vijijini ili wananchi wote waweze kumudu gharama za kuunganishiwa umeme, tofauti na ilivyokuwa hapo awali, ni jukumu lenu wananchi kutumia fursa hiyo kuunga mkono juhudi za serikali kwa kulipia gharama hizo”, Alisema Wakili Byabato.

Aidha alizungumzia hali ya kukatika kwa Umeme katika mkoa huo wa Kagera, ambapo alisema kuwa sababu kubwa ni Jiografia ya mkoa huo kuwa na Radi wakati wote ambazo zimekuwa zikisababisha uharibu miundombinu ya umeme.

Hali kadhalika umeme unaohudumia mkoa huo unasafiri umbali mrefu ikiwemo kutoka nchini Uganda na hivyo kupunguza nguvu yake na pia uchakavu wa miundombinu.

Aliweka wazi kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo, vifaa maalumu vinakufungwa katika miundombinu hiyo kupunguza ashari za Radi, na pia vifaa hivyo vitazuia tatizo likitokea eneo moja lisiathiri eneo jingine.

No comments