AMKA NA BWANA LEO 30

KESHA LA ASUBUHI

JUMATANO, JUNI, 30, 2021
SOMO: MTAZAMO WA KIKRISTO NA KUTAKA MAKUU 

Nimewaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu. Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. 

1 Yohana 2:14, 15. 



Roho yangu inahangaishwa ndani yangu ninapoona na kuhisi muda ulivyo mfupi ambao kwa huo yatupasa tufanye kazi. Kamwe hakujawa na mwonekano wa matokeo makubwa hivyo kututegemea sisi. Kamwe hakujawa na wakati ambapo vijana wa kila umri na kila nchi wamehitajika kutekeleza kazi ambayo yapasa ifanyike kama ilivyo sasa. 



Jamii inayo madai kwa vijana wa leo. Watu ambao wamekuwa wakisimama kwenye mstari wa mbele wa pambano, huku wakibeba mzigo wa joto la siku, watakuwa wakiondoka kwenye jukwaa la utendaji wa siku kwa siku. Wako wapi vijana wa kujaza mahali pao pale hawa waelekezaji wenye hekima na washauri watakapokoma kubeba mizigo yao? Majukumu haya sharti yatue mabegani mwa vijana. Basi ni muhimu kiasi gani, kwamba vijana wajielimishe, kwani majukumu haya yatahamishiwa kwao. 



Mwanangu, [William C. ], jiandae kutekeleza majukumu yako kwa uaminifu usio na waa. Natamani ningesisitiza kwa vijana kile ambacho wanaweza kuwa na kile wawezacho kufanya kama watahisi madai aliyo nayo Mungu kwao. Amewapatia uwezo, sio kutuama katika uvivu, bali kwa ajili ya kuimarisha na kuchangamsha kwa vitendo vya kiungwana. 



Willie, shauku yangu kubwa zaidi siyo kwamba wewe upate kuwa mkuu kulingana na viwango vya kidunia, bali mtu mwema, anayepiga hatua fulani kila siku katika kufikia viwango vya haki vya Mungu... 



Lazima tabia ijengwe. Hii ni kazi ya maisha. Hii ni kazi inayohitaji tafakuri na kufikiri. Akili ya utambuzi sharti itumike, bidii na ustahimilivu lazima vijengwe... Unaweza kutiwa moyo na wengine katika kazi yako, lakini kamwe, hawawezi kufanya kazi yako ya kushinda jaribu. Huwezi kuwa mwaminifu na mkweli, mchapa kazi na mwadilifu kwa ajili yao, wala wao hawawezi kuwa hivyo kwa niaba yako. Kwa namna moja ni lazima usimame mwenyewe, ukivipiga vita vyako mwenyewe. 



Hata hivyo, usifanye hivyo peke yako, kwani unaye Yesu na malaika wa Mungu walio tayari kukusaidia. Lakini ni wachache wanaofikia kile ambacho wanaweza kukifikia katika ubora wa tabia, kwa sababu hawaweki malengo yao juu.. Mafanikio na furaha haviwezi kujikuza vyenyewe. Ni matokeo ya mchakato wa kazi, tunda la maendeleo mazuri ya muda mrefu. 



—Barua ya 22, Juni 30, 1875,, kwa W. C. White, mwanawe wa umri wa miaka 20


No comments