ZANZIBAR KUTEKELEZA UJENZI WA BANDARI YA MAFUTA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar iko tayari kutekeleza mpango wa Ujenzi wa Bandari ya Mafuta katika eneo la Mangapwani.

Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Jijini Zanzibar baada ya kupokea Mpango wa ujenzi wa Bandari ya Mafuta (Master Plan) katika eneo la Mangapwani Mkoa wa Kaskazini Unguja, uliotayarishwa na Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman (OIA).

Amesema Serikali hivi sasa iko tayari kuanza majadiliano ya kina na wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika eneo hilo, baada ya kupokea mpango huo unaobainisha maeneo tofauti ambapo bandari tofauti zitajengwa.

Alisema wakati mchakato wa utayarishaji wa mpango huo ukiendelea
kuna wawekezaji kadhaa waliojitokeza na kuonyesha nia ya kuwekeza katika miradi tofauti, hivyo akatowa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kujitokeza na kuwekeza.

“Wafanyabiashara wa Zanzibar wana nafasi kubwa ya kuwekeza, ni vyema wakatumia fursa hiyo”, alisema.

Aidha, alitoa shukuran kwa Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman kwa kushirkiana kikamilifu na watendaji wa Serikali na hatimae kufanikisha kazi hiyo muhimu kwa wakati muafaka na kwa ufanisi mkubwa.


Aidha, Dk. Mwinyi alisema Zanzibar kama ilivyo kwa nchi za Visiwa, inategemea zaidi uwepo wa Bandari kubwa na za kisasa katika kuimarisha uchumi wake.

No comments