TIC YAANZISHA KITUO CHA MAWASILIANO KWA WAWEKEZAJI
Serikali imeendelea kufanya maboresho mbalimbali yenye lengo la kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini. Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) katika kuboresha na kurahisisha utendaji kazi wake kwa wadau wa uwekezaji kimeamua kuanzisha kituo cha mawasiliano kwa wawekezaji (Tanzania Investment Call Center) ili
kuwawezesha na kuwarahisishia wadau wa Uwekezaji kuweza kupata taarifa mbalimbali wanazo zihitaji kwa njia ya kupiga simu, barua pepe na mitandao ya jamii.
Taarifa zitakazopatikana katika kituo cha mawasiliano kwa wawekezaji ni pamoja na;
Taarifa za fursa za uwekezaji zilizopo nchini, taarifa za utaratibu wa kuwekeza nchini
pamoja na kupata leseni na vibali mbalimbali, wawekezaji kupata taarifa za maendeleo ya maombi yao ya vibali na leseni yaliyowasilishwa TIC na kutoa ushauri kuhusu sera, sheria na taratibu zinazohusiana na uwekezaji nchini.
Faida ya kituo cha mawasiliano kwa wawekezaji ni kupunguza muda na gharama kwa wawekezaji ambapo badala ya kufika TIC watakuwa wanapata huduma ya kuwasiliana wakiwa mahali popote walipo ndani na nje ya nchi.
Aidha, kituo hiki kitasaidia wawekezaji kupata taarifa sahihi na kwa wakati kutoka TIC na kuondoa usumbufu na taarifa potofu walizokuwa wanapata wawekezaji kutoka vyanzo ambavyo si sahihi (Vishoka).
Kituo cha mawasiliano cha wawekezaji kitarahisisha kupata mrejesho wa huduma zinazotolewa na TIC na taasisi nyingine zinazotokana na wawekezaji.
Namba za mawasiliano za kituo cha mawasiliano kwa wawekezaji ni: 0734 98 94 70, 0734 98 94 71 na 0734 98 94 72.
Aidha, Serikali kupitia TIC na wadau wake inatengeneza mfumo kwa ajili ya kuwekeza
Tanzania (Tanzania Single Window for Investment) ambapo mifumo yote inayotumika
na taasisi zinazohusika na utoaji wa vibali na leseni kwa wawekezaji katika eneo la One Stop Facilitation Centre lililopo TIC itaunganishwa ili kumwezesha mwekezaji kupata huduma zote kwenye mfumo mmoja.
Kituo cha mawasiliano kwa wawekezaji (Tanzania Investment Call Centre) kimezinduliwa na Katibu Mkuu wa Uwekezaji, Prof. Godius Kahyarara.
KUTOKA KITENGO CHA (TIC)
Post a Comment