BARUA YA SIMBA SC KWA UMMA NA KWA TFF

Klabu ya Simba inapenda kutoa tamko kuhusu kuahirishwa kwa mchezo wake dhidi ya Yanga, uliokuwa ufanyike jana Mei 8, 2021.

Mnamo majira ya saa saba mchana, tulipokea simu kutoka Bodi ya Ligi na Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) ikitueleza kuhusu mapendekezo ya kuahirishwa kwa mchezo huo kutokana na maelekezo ya Serikali. Muda mfupi baadaye, tulipokea taarifa rasmi ya kimaandishi juu ya uamuzi huo kutoka kwenye mamlaka hizo zinazosimamia mchezo wa soka nchini.

Pamoja na kusikitishwa na uamuzi huo, sisi kama Klabu tulikubali hasa kwa kuzingatia kwamba wote tunafanya shughuli zetu chini ya mamlaka hizo na tunaamini kwamba kama wameamua kuchukua hatua hiyo basi wanazo sababu za msingi hatukuhoji.

Tulitaarifiwa kwamba wenzetu Yanga nao walikuwa wamepata taarifa kama hiyo ambapo
walikubaliana na muda mpya wa mchezo kuanza. 

Katika kuheshimu na kutekeleza mabadiliko yale. Tulibadili ratiba zetu za ndani ikiwemo kusogeza mbele muda wa kupeleka timu uwanjani.

Hata hivyo, tulipofika uwanjani tulianza taratibu zote za kimchezo mbele ya wasimamizi wa mchezo akiwemo General Coordinator. 

Ghafla saa 12 tulitaarifiwa kwamba mchezo
umeahirishwa na hatukupewa sababu yoyote ya msingi inayohusiana na ahirisho hilo.

Tulishindwa kuelewa sababu ni nini, hasa tukizingatia kwamba maelekezo tuliyokuwa nayo
kutoka Bodi ya Ligi yalihusu kusogezwa mbele kwa muda wa mchezo kuanza kama ilivyokuwa
imeelekezwa na Serikali. 

Mkanganyiko huu ulitufanya tujiulize hili suala la kuahirisha mchezo limetokea wapi lakini hatukupata jibu.

Sote tunajua kitendo kilichofanywa na Yanga tafsiri yake ni kwamba wamegomea mchezo na adhabu yake ni kushushwa madaraja mawili na Simba kunufaika kwa kupewa alama tatu na magoli mawili. Mbali na hayo pia kitendo chao ni sawa na usaliti kwa nchi na Serikali, ambao ilitoa maelekezo maalum kusogeza mechi kwa masaa mawili zaidi.

Hivyo basi; kwa upande wetu tunaamini ahirisho lile la mechi limefanywa makusudi na Bodi ya Ligi kwa nia ya kuipendelea Yanga ambayo ilipaswa itii maagizo yao na ya TFF juu ya muda wa kuanza kwa mechi kama ilivyoelekezwa na Serikali na kisha kutujulisha sisi Simba imesikitishwa sana na uamuzi huo wa Bodi ya Ligi ambao unaonyesha dhamira ovu juu ya klabu yetu na jambo jingine linaloongeza mashaka katika kadhia hii ni kuiruhusu Yanga kuingia uwanjani kinyume na utaratibu wa muda maalumu unaoruhusiwa kabla ya kuanza kwa mchezo husika. Simba Sports Club; inaliona jambo hili limeratibiwa kiunazi na Bodi ya Ligi na inaomba
vyombo vyetu husika vilichunguze kiundani ili kubaini ukweli wake Sisi tunajiuliza; hivi Bodi ya Ligi, TFF na Serikali havina nguvu ya kimaamuzi kwa klabu ya mpira hadi igomee maelekezo yake? 

Na kisha Bodi ya Ligi ipinge maelekezo ya serikali
ya kusogeza muda wa kuanza mechi na yenyewe iamue kuahirisha mchezo bila kuzingatia
athari zinazoweza kujitokeza?

Klabu yetu imeamua kuziandikia barua mamlaka husika ili kupata ukweli wa jambo hili na baadaye ikiwezekana zichukue hatua stahiki. 

Mwisho Tunawapa pole washabiki wetu, wanachama wapenda soka na Watanzania wote kwa ujumla kwa misukosuko yote ya jana na tunaamini mamlaka zitatoa maelekezo ya kumaliza jambo hili kwa haki bila kumuonea au kumpendelea yeyote.

Tunawasihi washabiki wetu kuwa watulivu katika kipindi hiki, tunaamini haki yetu itapatikana
Imetolewa na Idara ya Habari
Simba Sports Club.

No comments