WAZIRI UMMY AAGIZA UJENZI WA HOSPITALI YA WILAYA MKINGA KUKAMILIKA KWA WAKATI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Ummy Mwalimu amemuagiza mkandarasi SUMA JKT kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mkinga ifikapo tarehe 30 Juni, 2021

Ametoa agizo hilo Leo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga, Mkoani Tanga.

Waziri Ummy amesema kukamilika kwa ujenzi wa Hospitali hiyo kutasaidia wananchi kutokutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika Hospitali ya Mkoa ya Bombo, Mkoani Tanga

Amesema kuwa tayari Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa Bajeti ya 2021/22 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali hiyo ambapo bilioni 1 kwa ajili ya kuongeza ujenzi wa miundombinu na milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba

Amesema kuwa Lengo la Serikali ni kuhakikisha inasogeza huduma bora za afya karibu na wananchi hivyo SUMA JKT ihakikishe inakamilisha ujenzi kwa wakati na unaendana na gharama halisi ya fedha zilizotolewa na Serikali.

Aidha amewaagiza viongozi wa Mkoa na Wilaya kuhakikisha wanasimamia ujenzi wa Hospitali hiyo ili ukamilike kwa wakati na kuhakikisha wanatoa vifaa kwa haraka.

Awali Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga ilipokea shilingi Milioni 500 ambazo hazikutumika kutokana na kupokelewa mwisho wa mwaka wa fedha kisha kupokea tena shilingi Bilioni moja ambazo ndizo zinaendelea na kazi kwa hivi sasa.

No comments