BARAZA LA MADIWANI KUPITISHA VIPAUMBELE VYA BARABARA ZA TARURA
Na Mathew Kwembe, Dodoma
Serikali imesema kuanzia mwaka ujao wa fedha utaratibu wa vipaumbele vya barabara zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini TARURA utapitishwa na Baraza la Madiwani.
Akihitimisha na kujibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia bajeti ya ofisi hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu amesema serikali imefanya uamuzi huo ili kuwapa fursa Madiwani kujadili vipaumbele vya matengenezo, maboresho pamoja na ujenzi wa barabara.
Amesema kuanzia mwaka ujao wa fedha Waheshimiwa Madiwani watakuwa na siku nne badala ya tatu za kujadili bajeti, kwa kuwaongezea siku moja ambayo itakatumika kujadili vipaumbele vya matengenezo na ukarabati wa barabara.
“Tumeongeza siku moja kabla ya zile siku tatu za Madiwani kujadili bajeti kuitumia kujadili vipaumbele vya matengenezo, maboresho pamoja na ujenzi wa barabara, na ikiwezekana Madiwani waende ‘site’ wakaone hizo barabara ambazo zinapendekezwa kujengwa na kufanyiwa maboresho,” amesema.
Uamuzi huo wa serikali unafuatia malalamiko ya Wabunge mbalimbali waliochangia hoja katika bajeti ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kuwa maamuzi ya barabara ipi ijengwe yamekuwa yakifanywa na Wataalamu wa TARURA katika ngazi ya mkoa,badala ya uamuzi huo ufanywe katika ngazi ya halmashauri.
Bunge limeidhinisha mapato na matumizi ya bajeti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika mwaka wa fedha 2021/22 ambapo jumla ya Shilingi Trilioni Saba Bilioni Mia Sita Themanini na Tatu Milioni Mia Tatu Ishirini na Tisa Mia Sita Arobaini na Nne Elfu na Mia Nane, (Tsh7, 683,329,644,800.00), kwa ajili ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Tume ya Utumishi wa Walimu, na Mikoa pamoja na Halmashauri zake 184.
Post a Comment