mafunzo ya watu wazima leo 7

LESONI, MACHI 7

SOMO: KUNUNUA KITU BURE? (ISAYA 55:1—7)



Soma aya hii: “Haya, kila aonaye kiu, njoni majini, Naye asiye na fedha; njoni, nunueni mle; Naam, njoni, nunueni divai na maziwa, Bila fedha na bila thamani!” (Isaya 55: 1). Je ni ukinzani gani unauona hapo?



Hebu fikiria kama ungechukua chakula na kusimama barabarani katika jiji kubwa na kuwatangazia wenye njaa na wasio na makazi walioko pale: “Haya, ninyi ambao hamna fedha, njoni, mnunue chakula na mpate kula!” Lakini wanawezaje kununua ikiwa hawana fedha? 



Hata hivyo, ikiwa utaongeza maneno, kama vile Isaya alivyofanya: “bila fedha na bila thamani (Isaya 55: 1), hoja inakuwa dhahiri zaidi. Isaya anawasihi watu wakubali msamaha (Isaya 55: 7) bure. Hata hivyo, neno kununua linasisitiza kwamba kile ambacho Mungu anawapa watu kukidhi mahitaji na matamanio yao ni cha thamani; hivyo, kukipokea kunahitaji muamala (uhamishaji wa kitu cha thamani). Mungu anatoa bure msamaha ndani ya mfumo wa uhusiano uliorejeshwa wa agano na watu wake, lakini sio kwa sababu ulikuwa bure kwake: Aliununua kwa bei kubwa ajabu, thamani iliyoloweshwa na damu ya Mtumishi wake mwenyewe. Ingawa ilikuwa bure, ilikuja pamoja na gharama ya kushangaza kwake. 



Je thamani ya wokovu wetu ilikuwa nini? Angalia 1 Petro 1:18, 19. Je mtazamo wa Isaya kuhusu wokovu unalinganishwaje na ule wa Agano Jipya? Waefeso 2:8, 9.



Isaya anaifunga injili katika Agano la Kale, nayo ni sawa na injili iliyomo katika Agano Jipya. Hakukuwapo na wokovu kwa njia ya matendo wa agano la kale;, ambao nafasi yake ilibidi ichukuliwe na wokovu wa agano jipya; wokovu kwa njia ya neema. Tangu ahadi ya Mungu kwa Adamu na Hawa ya Mkombozi (Mwanzo 3:15), kumekuwa na njia moja tu ya kufikia wokovu: kwa neema kwa njia ya imani (Wefeso 2:8); karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu (Warumi 6:23). 



Tangu Gilgamesh wa kale, ambaye alifanya matendo ya kishujaa akitafuta uzima wa milele bila mafanikio, hadi kufikia kwa waigizaji wa kisasa wenye imani kuwa roho ya marehemu huingia katika mwili wa mtu mwingine na kuzaliwa upya, watu wamejaribu njia zote tofauti kufikia wokovu, lakini zote hazizai matunda. Hii ndio sababu inabidi wapate kumjua Yesu na yale ambayo ameyatenda kwa ajili yao pale Msalabani. 



Wokovu ni bure kwa kuwa hakuna kitu chochote tunachoweza kufanya ili kuupata. Kazi zetu haziwezi kuwa nzuri kiasi cha kutosha kutuokoa. Hata hivyo, wakati uo huo, unaweza kutugharimu kila kitu. Hiyo inamaanisha nini? Angalia, kwa mfano, Mathayo 10:39, Luka 9:23, 14:26, Wafilipi 3: 8.

No comments