amka na Bwana
KESHA LA ASUBUHI
Jumatatu 08/03/2021
*KILE KINACHOFANYWA NA UPENDO*
*Nitamsifu BWANA muda ninaoishi; Nitamwimbia Mungu wangu ningali ni hai.* *Zaburi 146:2*
Kwa muda wa nusu karne nimekuwa mjumbe wa Bwana, na kwa kadiri maisha yangu yanavyoendelea ndivyo nitakavyoendelea kutoa ujumbe anaonipatia Mungu kwa ajili ya watu wake. Sijichukulii utukufu, katika ujana wangu Bwana alinifanya mjumbe wake, kuwasilisha kwa watu wake shuhuda za kutia tumaini, maonyo, na kukemea. Kwa miaka sitini nimekuwa nikiwasiliana na wajumbe wa kimbingu, na kwa kudumu nimekuwa nikijifunza kwa habari ya mambo ya kiungu, na kwa habari ya namna ambayo Mungu hutenda kazi kwa kudumu kuzileta nafsi kutoka katika makosa ya njia zao katika nuru ya Mungu...
Ninampenda Mungu. Ninampenda Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, na ninahisi mvuto mkali kwa kila nafsi inayodai kuwa mtoto wa Mungu. Nimedhamiria kuwa wakili mwaminifu kwa kadiri Mungu atakavyoendelea kuyahifadhi maisha yangu. Sitashindwa wala kukatishwa tamaa.
Lakini kwa miezi mingi moyo wangu umekuwa ukipitia mateso makali kwa habari za wale waliopokea madanganyo ya Shetani na kuwapelekea wengine hayo, na kufanya kila tafsiri inayowezeka kwa namna tofauti tofauti kuharibu imani katika ujumbe wa injili katika kizazi hiki cha mwisho, na katika kazi ya pekee ambayo Mungu amenipatia kuifanya. Najua kuwa Bwana amenipa kazi hii, na sina udhuru wa kutoa kwa kile nilichofanya.
Katika uzoefu wangu kwa kudumu ninapokea ushahidi wa nguvu ya Mungu inayotenda miujiza itegemezayo katika mwili na nafsi yangu, niliyoiweka wakfu kwa Bwana. Mimi si mali yangu mwenyewe; nimenunuliwa kwa thamani. Na nina uthibitisho wa utendaji wa Bwana kwa niaba yangu kwamba ni sharti nithamini neema yake nyingi. *Ninampenda Bwana; ninampenda Mwokozi wangu, na maisha yangu yote yako mikononi mwa Mungu. Kwa kadri anavyonitegemeza, nitatoa ushuhuda thabiti.*
*Kwa nini nilalamike? Mara nyingi sana Bwana ameniinua kutoka katika ugonjwa, kwa namna ya ajabu amenitegemeza, ambapo siwezi kabisa kutilia shaka. Nina vithibitisho vingi vya wazi vya baraka zake za pekee, ambazo siwezi kuzitilia shaka. Hunipa uhuru wa kusema kweli yake mbele ya idadi kubwa ya watu.*
*TAFAKARI NJEMA MUNGU AKUBARIKI MPENDWA*
Post a Comment