mtoto mtundu

VITOTO VYA SKUIZI!! 

Kweli Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo!!

Juzijuzi hapa nilimtembelea rafiki yangu niliesoma nae secondary Kizwite. Jamaa anaishi mitaa ya Kasisiwe, maisha yake si haba. Huwezi kumfananisha na sisi wa Chanji-Soweto. Jamaa anaishi na mkewe, wana katoto kadogo ka miaka kama mitano au sita hivi. Katoto kao  kanaitwa kaJunia, sijui Junya, hivyo hivyo yaani. Kanasoma izi shule za Nasari, sijui English midiamu hizi. Kiujumla jamaa anaishi maisha ya kwenye TV na familia yake. 

Yaani tangu naingia mle ndani mwake, haka katoto hakajui kusema "mama" wala "baba". Kanajua kusema Dadi na Mami tu. Basi jamaa yangu anajiona mjaaaanja!! Basi Kabwana mdogo hako hakakaripiwi wala kukatazwa chochote.

Nilipofika tu nilishtushwa na mwenendo wa hako kabwana mdogo, dada wa kazi ambae nilimleta mimi kutoka kijijini kwetu mwaka juzi akaanza kunishangaa  na kusema kuwa hayo kanayoyafanya ni madogo sana. Kuna siku kalimvua baba yake taulo alipokuwa anatoka bafuni tena mbele za watu, jamaa akaishia kusema tu, "No Junia No...! This is bad!” Huku babaake akichekacheka huku anakasifia, "Tatizo la huyu mtoto ni kwamba ana akili za kikubwa” Daah!! Hii stori kutoka kwa dada wa kazi iliniacha mdomo wazi.

Ene wei, siku hiyo jamaa akanikaribisha kwake, basi kwa kweli ilikuwa kero, mara Junia kaleta mpira sebuleni kisha anaupiga mbele yetu,  anaangusha vitu, mara anatupiga usoni na
mpira na anaangaliwa tu. Jamaa anaishia tu kusema, "Junia no! This is bad Junia", lakini huyo Junya hasikii, kwaanza ndo anapanda juu ya meza, mara kabatini, yaani kero tupu. 

Jamaa yangu na mke wake utadhani wamelogwa, wanakenua tu meno, "No Junia no!!". Mara kakaniparamia na kutaka kunivua miwani yangu, "Kwa ustaarabu wa nyumba ile na mie nikatoa kauli ya kinafiki, "No Junia No, this is bad!!" Muda huo kulikuwa kuna taarifa ya habari, lakini hicho kijunya kikang'ang'ania kiwekewe katuni. Jamaa akakiwekea. Basi bora hata kingekuwa kinaangalia hizo katuni, muda wote kinataka kupakatana tu hadi kinachomoa shati langu nililochomekea vizuri wakati naingia mle ndani. Kama dakika kadhaa hivi kupita, mama Junia akaingia jikoni, baba Junia nae akaenda chumbani kidogo, hivyo sebuleni tukabaki mimi na hiki kidude kisichokuwa na chembe ya adabu.

Si kikaanza vimaswali vya maudhi...! Eti kinaniuliza, "Leo umekuja kula kwetu?" "Kwenu
mna TV kama hii? Babaako anakuleteaga chokleti?" Kikaanza mchezo wa kunitemea mate huku kinacheka. Mwanzo nilijua labda kitaacha. Kadri ninavyojifuta yale mate, ndivyo ambavyo kinaona kama ni mchezo flani wa kuburudisha. Mamaake akiwa jikoni akaskika akisema, "No Junia, don du dhat tu yuwa anko!!" Mara kinipige na rimoti usoni, mama yake anapiga tu kelele akiwa jikoni, "Junia yua veri bad", chenyewe kinajibu, "Nooo mamiiii!!"

Kilipojichanganya ni pale kilipoanza kunipanda kichwani na kunivuta nywele zangu za kipilipili. Nikaona sasa hii ni dharau. Basi nilikishika mkono wake kwa nguvu. Si unajua tena mikono imara ya sisi mafundi magari!!? Nikakitolea macho na kukifinya vizuri mashavu yake. Kwanza hakikuamini kilichokiona, nadhani kiliifananisha mikono yangu na ile ya King Kong wa kwenye muvi. Kilijaribu kujitoa mikononi mwangu lakini nilikikaza kisawasawa mashavu yake. Kikatoa macho kama kinataka kufa. Kikaniangalia usoni huku hakiamini kuwa kinafinywa na binadamu aliye hai. Huku bado nimekishika mashavu yake, nikakiambia kwa sauti ya chinichini yenye kitisho... "We Junya ukinisogelea tena nakukata masikio kabisa!!" kisha nikakiachia kiondoke. 

Eeh bwana wee... kilitimka mbio mle sebuleni huku mkojo unakitiririka. Kikaelekea jikoni kwa mama yake. Kufika huko nilitegemea kitaanza kulia kwa nguvu, cha ajabu kikawa kimya. Mama yake akakiuliza "Junia umefanya nini tena baba?" Kikawa kimya. "Junia what happened?" Bado kikawa kimya, mama yake akaja sebleni huku chenyewe kimejificha nyuma ya gauni la mamaake. Mamaake akaniuliza, "Shem huyu kafanya nini?" Na mimi nikajibu kwa sauti ya mtu asiye na dhambi kabisa... "Shemeji wala sijui kabisa, nimeona tu katimka hapa kaja huko". Baada ya hapo kukawa na displini mle ndani, tukala na kuzungumza bila fujo.

Baba Junia kila mara alimwangalia mwanae na kumuuliza, "Junia, ayu siki? Unaumwa?" Junia alinitupia jicho mwenyewe bila kujibu kitu, nadhani ile ahadi yangu ya kumkata masikio ndio ilimkosesha raha. Mpaka naondoka, nyumba ilijaa ustaarabu wa kutosha.
Wengine maisha ya kwenye video hata hatuyajuagi!! Sasa sijui nilikosea wapi wadau!!???

No comments