amka na Bwana leo 16
KESHA LA ASUBUHI
JUMANNE, FEBRUARI, 16, 2021
SOMO: MUNGU HUCHUKIA UDANGANYIFU
Piga kelele usiache, paza sauti yako kama tarumbeta uwahubiri watu wangu kosa lao, na nyumba ya Yakobo dhambi zao.
Isaya 58:1.
Unafiki kwa namna ya kipekee ni kosa kwa Mungu. Idadi kubwa ya wanaume na wanawake wanaodai kuijua kweli hupendelea jumbe laini. Hawataki dhambi na kasoro zao ziletwe mbele yao. Wanataka wahubiri wanaochukuliana nao, ambao hawataamsha kusadikishwa kwa kusema kweli. Wanachagua watu watakao wapendeza, na kwa upande wao wanamsifu mno mhubiri ambaye ameonesha roho “njema” huku wakimshutumu mtumishi mwaminifu wa Mungu....
Wengi humsifu mhubiri anayehubiri kuhusu neema na rehema na upendo wa Yesu, ambaye hasisitizi hasa majukumu na wajibu, ambaye haonyi juu ya hatari ya unafiki, au kusema juu ya hofu ya ghadhabu ya Mungu.
Kazi ya Mungu ni ya dhati na thabiti, juu kabisa ya udanganyifu na unafiki. Wachungaji wake wa kweli hawatamsifu na kumwinua mwanadamu. Watakuja mbele za watu kwa wazi na “Hivi ndivyo asemavyo Bwana, Mtakatifu wa Israeli.” Watabeba ujumbe wake, haidhuru watu wausikie au waudharau. Ikiwa watu wanadharau Neno la Mungu, na kutumainia ukandamizaji, unafiki, na kupenda anasa za dunia, ni lazima watangaziwe maonyo ya Mungu dhidi yao, ili ikiwezekana waamshwe kutubu. Ikiwa wanakiburi kiasi cha kutokuwa tayari kutubu, na kukiri makosa yao, kumgeukia Mungu, kuukaribisha wokovu wake na kupokea ukubali wake, Bwana ataondoa nuru yake toka kwao na kuwaacha watembee katika njia walioichagua.
Wale wanaowabana wajumbe waaminifu wa Mungu kwenye kona, wanaowakatisha tamaa, wanaosimama kati yao na watu, ili ujumbe wao usipate mvuto ambao Mungu amekusudia uwe nao, watawajibika kwa ajili ya udanganyifu na maasi yanayokuja kanisani kama matokeo ya kazi yao. Wana jukumu la kutisha la kutoa hesabu mbele za Mungu.
Baada ya Bwana kuwaonya kwa kurudia rudia watu wake, na bado wanakataa kuisikia sauti yake, na hawataki kuelekezwa, hatia yao itakuwa ya kuchukiza kwake ajabu. Rekodi ya uasi wao inaandikwa kwenye kitabu mbele zake, naye atawakabili wakati hukumu itakapowekwa na vitabu kufunguliwa.
Post a Comment