mafunzo ya watu wazima leo 26

LESONI, JANUARI 26

SOMO: FIMBO YA HASIRA YA MUNGU (ISA. 9:8—10:34)



Sehemu hii huelezea Isaya 9:1—5, ambayo hutabiri ukombozi wa watu wenye huzuni, wanaotaabika ambao walitegemea ibada ya mashetani na kujikuta wamekuwa mateka wa wanajeshi na wahanga wa uonevu: “fimbo yake yeye aliyemwonea, kama katika siku ya Midiani” (Isa. 9:4). 



Soma mateso ya watu wa Mungu kama yalivyooneshwa katika aya zilizopo hapo juu. Linganisha na laana katika Walawi 26:14—39. Kwa nini Mungu aliwaadhibu watu Wake hatua kwa hatua badala ya mara moja? Jambo hili linaashiria nini kuhusu tabia na malengo Yake?



Ikiwa Mungu angetaka kuwaangamiza watu Wake, angeweza kuwatoa kwa Waashuru mara moja. Lakini Yeye ni mvumilivu, “maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba” (2 Pet. 3:9). Kama kipindi cha “waamuzi,” Mungu aliwaacha watu wa Yuda na Israeli wapate matokeo ya upumbavu wao ili waelewe kile walichokuwa wakikifanya na wawe na nafasi ya kufanya uchaguzi bora zaidi. Walipong’ang’ania uovu na kuwa na mioyo migumu dhidi ya miito aliyoituma kwa njia ya wajumbe Wake, alizidi kuondolea ulinzi Wake. Lakini waliendelea kuasi. Mzunguko huu ulijirudia-rudia na kuwa endelevu mpaka Mungu akawa hana cha kufanya. 



Soma Isaya 9:8—10:2 yote. Watu wana hatia ya dhambi gani? Wamezitenda dhidi ya nani? Ni nani wana hatia miongoni mwao?



Tunachokiona hapa, kama kinavyoonekana katika Biblia, ni uhalisia wa uhuru wa kuchagua. Mungu aliwaumba wanadamu wakiwa huru (Ilimpasa kufanya hivyo; vinginevyo, wasingeweza kumpenda), na uhuru huhusisha uwezekano wa kukosea. Na ingawa mara nyingi Mungu hutusihi kwa kutufunulia upendo Wake na tabia Yake, ataruhusu pia tukabiliwe na matunda ya chaguzi zetu mbaya; yaani, maumivu, mateso, hofu, machafuko, na kadhalika, yote hayo ili kutusaidia tugundue kile ambacho hutokea tunapomwacha. Na bado, hata hivyo, mara nyingi mambo haya hayawasaidii watu kuacha dhambi na kumrudia Bwana. Uhuru wa uchaguzi ni jambo la ajabu; tusingeweza kuwa wanadamu bila kuwa nao. Hata hivyo, ole wao, wanaoutumia vibaya. 



Ni kwa jinsi gani Mungu ametumia mateso katika maisha yako kubadilisha mwelekeo wako potovu? (Au, pengine, bado hujaelewa)

No comments