mafunzo ya watu wazima leo 14

LESONI, JANUARI 14

SOMO: “MUNGU YUKO PAMOJA NASI”! (ISA. 7:14) 



Kama majina ya watoto wa Isaya yalivyo (Shear-yashubu, “Waliosalia watarudi,” na Maher-shalal-hash-bazi, linalomaanisha "mali ya wizi ni ya mbio, mawindo ni ya ghafla") jina Imanueli lina maana. Maana yake sisisi ni "pamoja nasi Mungu." Lakini tafsiri inayokubalika zaidi “Mungu pamoja nasi” inakosa kitu muhimu. 



Kama majina mengine ya Kiebrania ya aina hii ambayo hayana vitenzi, kitenzi “yuko” lazima kiongezwe, kwa kuwa hakipo katika Kiebrania. Hivyo, Imanueli lazima litafsiriwe “Mungu yuko pamoja nasi” (linganisha na maneno hayo hayo katika Isa. 8:10), kama vile jina "Yesu" (Kigiriki, na kifupi cha Kiebrania Yehoshua, au Yoshua) humaanisha “Bwana ni wokovu,” na kitenzi tena kikiwa kimeongezwa (linganisha na Isaya, ambalo humaanisha, “wokovu wa Bwana").



Lakini jina “Imanueli” siyo maelezo ya jambo la kufikirika; ni tamko linalohusu ahadi inayotimizwa sasa hivi: "Mungu yuko pamoja nasi"!



Ni nini maana ya ahadi kuwa Mungu yuko pamoja nasi? 

Hakuna hakika na faraja yenye nguvu zaidi kuliko hii. Mungu haahidi kuwa watu Wake hawatapata matatizo na maumivu, lakini anaahidi kuwa atakuwa pamoja nao. Mtunga Zaburi anasema: "Nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji" (Zab. 23:4). 



"Mungu anasema: ‘Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza’ (Isa. 43:2). 



“Bwana alikuwa wapi wakati Wababeli walipowatupa marafiki watatu wa Danieli motoni? Alikuwa pamoja nao (Dan. 3:23—25). Na Bwana alikuwa wapi wakati wa taabu ya Yakobo alipopigana mieleka mpaka kukapambazuka? Yakobo alikuwa kiganjani Mwake, alikuwa karibu sana kwa kadiri ilivyowezekana (Mwa. 32:24—30).



"Hata wakati ambao Bwana haonekani kwa macho hapa duniani, anapitia uzoefu wa watu Wake pamoja nao. Bwana alikuwa wapi wakati watu waovu walipomwua Stefano? 'Alisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu' (Matendo 7:55). Lakini wakati Yesu alipopaa mbinguni, 'aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu' (Ebr. 1:3). Kwa nini alisimama wakati Stefano yuko katika mateso, akiwa karibu kuuawa kwa kupigwa mawe? Kama alivyosema Morris Venden, 'Yesu asingemudu kuendelea kukaa!" —Roy Gane, God’s Faulty Heroes (Hagerstown, Md.: Review and Herald Pub. Assn., 1996), uk. 66.



Ingawa tumeahidiwa kuwa “Mungu yuko pamoja nasi,” kwa nini bado tunakabiliana na majaribu na mateso makali? Kujua kuwa Mungu yuko pamoja nasi kunatusaidia nini? Fafanua jibu lako.

No comments