BAVICHA WAJIPANGA KUWAZIKA MDEE NA WENZAKE
BARAZA la Wanawake la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA), linapanga mkakati mzito unaolenga kumzika kabisa kisiasa, aliyekuwa mwenyekiti wao wa taifa, Halima James Mdee. Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam
Taarifa kutoka ndani ya Chadema zinasema, wanawake wa chama hicho, wanapanga “kumalizana na Mdee,” wakati wa maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani, yaliyopangwa kufanyika kitaifa, mkoani Iringa.
Wanawake wa Chadema, wamekuwa wakihamasishana kujitokeza kwa wingi kwenye maadhimisho hayo, ili kuudhihirishia ulimwengu na baadhi ya viongozi wakuu wa chama hicho, kuwa “Bawacha bila Mdee, inawezekana.”
Mdee anatuhumiwa kushirikiana na Tendega, Bulaya, Agnesta na Kunti, kupeleka majina Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Bunge, ili hatimaye wateuliwe na kuapishwa kuwa wabunge.
Katika kutekeleza mradi huo, Mdee anaoenakana kuongea na baadhi ya viongozi wandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bunge, NEC, pamoja na baadhi ya watu walioko “kwenye mfumo,” ili kufanikisha dhuluma dhidi ya wanawake wa Chadema.
Devota Minja, Mwenyekiti wa Bawacha mkoa wa Morogoro
Hatua ya Mdee kuwafanya baadhi ya maswahiba zake kuwa wabunge, imewanyima fursa wanachama wa chama hicho wenye sifa zaidi ya “waliobebwa na Mdee” nafasi ya kuwa wabunge.
Wengi walioumizwa na hatua hiyo, ndiyo wanaohamasishana kukutana Iringa, “ili kuonyesha Bawacha ni kubwa kuliko mtu.”
Katika mkakati wa kummaliza Mdee kwa kumuonyesha chama hicho ni taasisi iliyokamilika, wanawake hao wa Chadema, wameanza kuchangishana fedha kutoka mifukoni mwao, ili kuhakikisha maadhimisho hayo ya Iringa yanafana.
Tayari wanachama kadhaa wa Bawacha na hata wale wasiokuwa wanachama wa baraza hilo, wameanza kuchangia majimbo yao, ili yaweze kukusanya wanawake na kuwafikisha Iringa.
Mathalani, mwenyekiti wa Chadema katika jimbo la Segerea, jijini Dar es Salaam, Patrick Asenga amesema, wanachana na viongozi wa jimbo hilo, wameanza michango itakayowezesha kupatikana kwa zaidi ya Sh.1.2 milioni, zitakazotumika kupeleka wanawake katika tamasha hilo.
#BinagoUPDATES
Post a Comment