amka na Bwana leo 22

*KESHA LA ASUBUHI.*

Ijumaa, 22/01/2021.

*ANGALIA KIOLEZO.*

*Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu. Zaburi 119:105.*

▶️Mtendakazi wa Mungu hajaachwa bila kiolezo. Amepatiwa mfano ambao, ukifuatwa, utamfanya kuwa tamasha kwa ulimwengu, kwa malaika na kwa wanadamu. Anatakiwa kumtukuza Mungu kwa kubeba malengo na makusudi yasiyo ya kibinafsi. Bwana anatambua asili ya mwanadamu, naye ameweka mbele yake sheria za ufalme wa mbinguni, ambazo anapaswa kuziheshimu na kuzitii. Anatweka Biblia katika mikono yake kama kitabu cha mwongozo kitakachomwonesha kilicho kweli, na kile anachopaswa kufanya ili kuurithi uzima wa milele. Kitabu hiki huvuta fikra zetu toka mambo ya muda mfupi kwenda katika uhalisia wa kiroho. Humwambia mwanadamu, kwamba japo ameanguka na ni mwenye dhambi, anaweza kuwa mwana wa mfalme na mfalme katika nyua za mbinguni, mrithi wa Mungu na mrithi pamoja na Kristo. 

▶️Mungu huona mwelekeo wa mwanadamu ulivyo na nguvu katika kujilimbikizia hazina za duniani, na katika barabara kuu na ndogo za maisha yake sauti yake husikika, “Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake? (Marko 8:36). “Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako.” (Mathayo 6:19—21). 

▶️Wajumbe wa Mungu wamepewa agizo kubeba kazi ile ambayo Kristo aliifanya akiwa katika dunia hii. Wanapaswa kujitoa kwa kila nyanja ya huduma aliyoitenda. Kwa bidii na kwa dhati wanapaswa kuwajulisha watu juu ya utajiri usiofikika na hazina zisizo na kikomo za mbinguni. Wanapaswa kujazwa kwa Roho Mtakatifu. Wanapaswa kuzirudia ahadi za bure za mbingu za amani na msamaha. Wakielekeza katika malango ya mji wa Mungu watasema, “Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake” (Ufunuo 22:14). 

▶️ *Mungu anatarajia kila mmoja kumtendea kazi kulingana na uwezo wake tofauti tofauti. Shughuli ya mwanadamu haipaswi kukandamizwa, bali kutakaswa na kupatiwa mwelekeo sahihi.*

*MUNGU ATUBARIKI TUNAPOTAFAKARI NENO LAKE.*
🙏🙏🙏🙏

No comments