amka na Bwana leo 16
KESHA LA ASUBUHI
JUMAMOSI, JANUARI, 16, 2021
SOMO: KITUO CHA UMEME CHA ULIMWENGU
Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.
Isaya 41:10.
Yesu Kristo ndiye mwalimu mkuu kuliko wote wa ulimwengu. Nimejaribu na kuthibitisha ushahidi uliobarikiwa wa jambo hili. Amenifanya kuwa mjumbe wake, kutangaza kweli kuu za kiroho kwa maelfu mengi.... Ninatamani mno kuwasilisha maelekezo yake ili wengi waongozwe kwenda Kwake. Sina shaka na uongozi wake, na ninajua kwamba ninategemezwa na Yeye aliyewaamuru wanafunzi wake wasonge mbele na kuutangaza ujumbe wa injili, “Na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari” (Mathayo 28:20).
Tangu mwaka 1844 nimekuwa nikihusika katika kazi ya jumuia. Mara zote nimetiwa nguvu na Bwana. Ninatambua kuwa ninapewa uwezo toka juu, ukinipa ufanisi wa kimwili, kiakili, na kiroho. Nina uhakikisho mkamilifu kuwa Kristo ananipa neema yake itegemezayo na ushahidi kwamba yeye ndiye nuru ya ulimwengu. Ninatambua uweza wake. Ninatamani kufanya kila ninaloweza kwa ajili yake nikingali hai. Ninataka, kwa imani tulivu na kamilifu, kusalimisha utunzwaji wa nafsi yangu kwa Mungu dhidi ya siku hiyo. Wakati kazi yangu hapa itakapokoma, nitapumzika. Kulala katika Yesu si jambo la kuogofya kwangu. Katika asubuhi ya ufufuo nitamwona kama alivyo....
Hebu tuhakikishe kuwa tunaweka sawa mambo yetu na Mungu, ili kwamba Bwana aweze kutufundisha na kutuongoza, na kuyafunua mapenzi yake kwetu. Tafadhali zingatia mambo haya. Na hebu tutumie muda wetu mwingi na Mungu katika maombi. Bwana ni msaada wetu na nguvu na ngome. Ikiwa tutaenda kwa unyenyekevu na Mungu, tukilicha na kulitukuza jina lake, atakuwa katika mawazo na mioyo yetu, nasi tutafanywa tufanane na sura yake. Hebu tuichunguze kwa bidii mioyo yetu wenyewe, ili tupate ile hekima ambayo Mungu pekee ndiye anaweza kuitoa.
Hebu tukumbuke kwamba mashaka ni hatari. Yakiendekezwa, yanasababisha kutokuamini.... Watu wetu wote wanahitaji sasa kutafuta kumwagiwa Roho Mtakatifu. Tusiingie katika ugomvi, lakini weka kando mafarakano na mapambano, na jitahidi kujibu ombi ambalo limeandikwa katika sura ya kumi na saba ya Yohana. Ninawasihi mwombe, omba, kwa moyo na roho na sauti.
Post a Comment