viongozi wa Dini wamteta Askofu Gwajima kuwa mgombea wa Ubunge
MIZANI: UASKOFU NA UBUNGE
Maamuzi ya askofu Dr Josephat Gwajima kujitosa kugombea nafasi ya ubunge yamewashtua wachamungu.
Wapo wachamungu ambao wamefurahishwa na hayo maamuzi na wapo wengine ambao wamehuzunishwa! Kila kundi lina mtazamo wake uliopelekea mshtuko huo kuwa hasi au chanya.
Lakini pia maamuzi yake yameibua maswali kwa watu wanao fikiri.
Je, kimaandiko ni halali Askofu kugombea urais, ubunge au udiwani?
Jibu la harakahara ni NDIO au HAPANA!
Kuna wakati jibu linaweza kuwa ni NDIYO na kuna wakati jibu linaweza kuwa ni HAPANA - kulingana na wakati husika.
" Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake ... " MUHUBIRI 3:11
Kwa wakati huu askofu Dr Josephat Gwajima kugombea ubunge SIO HALALI - kimaandiko kwa mchanganuo ufuatao:
Kwa mazingira yaliyopo sasa katika nchi yetu wanachama wa vyama vya siasa wengi wana uhasama (uadui). Wanashambuliana kwa mawe, wanachomeana ofisi mpaka wanatishiana kuuana!
Watu wa namna hiyo wanahitaji MPATANISHI ambaye hafungamani na chama cho chote cha kisiasa. Mtu ambaye hana agano na chama cho chote cha kisiasa!
Huduma hiyo ya upatanisho Mungu ametupa sisi tunaomwamini akiwemo askofu Gwajima.
" ... naye alitupa huduma ya upatanisho ... ametia ndani yetu neno la upatanisho ... " 2 KORINTHO 5:17 - 21
Hivyo viongozi wa dini na kila mwana wa Mungu hatupaswi kufanya agano lo lote na upande unaopingana na upande mwingine - ili kusudi tuweze kufanya upatanisho wa pande hizo hasimu!
" Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu. " MATHAYO 5:9
Danieli, Yusufu na Daudi waliongoza serikali ambazo zilikuwa hazina makundi yanayopambana! Wote walikuwa katika serikali zenye chama kimoja!
Kanisa lisipokuwa makini litaipoteza chumvi yake - na hakuna mtu atakayeliamini tena, hata wakati ambao litakuwa linahitajika sana katika kufanya maamuzi ndani ya nchi!
" Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. " MATHAYO 5:13
Mchungaji B.M. Mwasula
General Overseer - PCT Headquarters
Je una taarifa ya kusisimua kuhusu dini unataka tuchapishe,tafadhali tuma kupitia whatspp 255759701713
Post a Comment