amka na Bwana

*KESHA LA ASUBUHI.*

Jumapili 02 Agosti 2020.

*UWE NA JUHUDI KATIKA MATENDO MEMA.*

*_Ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema. Tito 2:14._*

▶️Wafuasi wa Kristo wamekombolewa kwa ajili ya huduma. Bwana wetu anafundisha kwamba kusudi la kweli la maisha ni huduma. Kristo mwenyewe alikuwa mfanyakazi, na kwa wafuasi wake wote Yeye hutoa sheria ya huduma—huduma ya kumtumikia Mungu na wanadamu wenzake. Hapa Kristo amewasilisha kwa ulimwengu dhana kuu ya maisha kuliko vile walivyowahi kujua. Kwa kuishi kuwahudumia wengine mwanadamu huletwa katika uhusiano na Kristo. Sheria ya huduma inakuwa kiungo kinachounganisha kwa Mungu na kwa wanadamu wenzetu. 

▶️Kwa watumishi Wake Kristo anatoa "mali Yake" —kitu ambacho kinapaswa kutumiwa kwa ajili Yake. Yeye humpa "kila mtu kazi yake." Kila mtu anayo nafasi yake katika mpango wa milele wa Mbingu. Kila mmoja anapaswa kufanya kazi kwa kushirikiana na Kristo kwa ajili ya wokovu wa roho. Kama ambavyo kwa hakika zaidi mahali pameandaliwa kwa ajili yetu katika makao ya mbinguni ndivyo pia mahali maalumu pameandaliwa hapa duniani ambapo tunapaswa kufanya kazi kwa ajili ya Mungu… 

▶️Na wale ambao wanataka kuwa watendakazi pamoja na Mungu ni lazima wajitahidi kwa ajili ya kufanikisha ukamilifu wa kila ogani ya mwili na ubora wa akili. Elimu ya kweli ni maandalizi ya nguvu za kimwili, kiakili na kimaadili kwa ajili ya utendaji wa kila wajibu; ni mafunzo ya mwili, akili, na roho kwa ajili ya huduma takatifu.... 

▶️Kwa kila Mkristo Bwana anahitaji ukuaji katika ufanisi na uwezo katika kila mwelekeo. Kristo amelipa mishahara yetu, kwa damu na mateso Yake, ili ajipatie huduma yetu ya hiari. Alikuja katika ulimwengu wetu apate kutupa mfano wa jinsi tunavyopaswa kufanya kazi na ni roho gani tunapaswa kuiingiza katika kazi yetu. 

▶️Anatamani tupate kuonesha jinsi tunavyoweza kuendeleza kazi Yake kwa ubora kabisa na kulitukuza jina Lake ulimwenguni, tukimvisha taji ya heshima, na upendo mkubwa na ibada, Baba ambaye "aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele."

*MUNGU AKUBARIKI UNAPOTAFAKARI NENO LAKE.*
🙏🙏🙏🙏

No comments