MTI WA UZIMA ;
By Pastor Mirambo's Son
SOMO : MTI WA UZIMA.
Utangulizi.
Bwana Mungu alipoiumba nchi, aliumba pia bustani akaiita jina lake Bustani ya Eden.Katika bustani hiyo ilikuwepo pia miti miwili, mti wa kwanza ni mti wa Uzima na mti wa pili ni mti wa ujuzi wa mema na mabaya!
Adamu alipoumbwa aliwekwa katika bustani hiyo, na akapewa masharti kwamba ili aishi bila kufa anatakiwa asile matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya! Kwamba siku akila matunda ya mti huo hakika atakufa! Masharti haya Adamu aliyafuata siku zote kabla ya Hawa kuwepo. Basi Mungu alipoona ni vema Adamu apate msaidizi wa kufanana naye akamletea mwanamke kutoka katika moja ya ubavu wake! Adamu akampenda mkewe! Akampa masharti kwamba Mungu amewakataza kula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya!
Lakini Hawa alipokuwa mbali na mumewe, Nyoka akamdanganya akala tunda la mti uliokatazwa na akampelekea mumewe naye akala ndipo mauti ikaingia duniani.
"Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.
Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya.
Bwana Mungu akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya."
(Mwanzo 2:7-9)
Kwa hiyo kulikuwa na miti miwili, mti uletao Uzima na mti uletao mauti.
"Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako;"
(Kumbukumbu 30:19)
Kwa hiyo Adamu na mkewe wakala matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, kwa hiyo badala ya kuchagua uzima wakachagua mauti, badala ya kuchagua baraka wakachagua laana!
Ndiyo siku mabaya yalipoikumba dunia, ndiyo siku magonjwa yaliingia !
Ndiyo siku uadui uliingia!
Ndiyo siku uzao usiomtii Mungu uliingia duniani nk.
Hawa alidanganywa na Nyoka(shetani baba wa uongo)
Akautamani huo mti akala
"Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala."
(Mwanzo 3:6 )
Kwa hiyo dhambi hutamanisha ! Ni kweli unatamani kufanya uzinzi lakini kumbe mauti inakuita, ni kweli unatamani kuvaa kimini ili upate wachumba wengi kumbe unaenda kuambulia ukimwi! Ni kweli umetamani kupata mali kwa haraka kumbe unaenda kutolewa kafara, siku zote tambua shetani hushawishi!! Usifikiri kwamba hawa hakuwa na akili , unapaswa kujua kwamba shetani alimshawishi! Macho yake yakaelekea huo mti akaona unapendeza kumbe anapokea mauti! Ni kweli watumishi wa Mungu wamekuhubiria uache uzinzi, uache kuvaa nusu uchi lakini shetani ameziba ameziba masikio yako, yawezekana ni mama mchungaji au ni mtumishi unahudumu kanisani, lakini utukufu humpi Mungu bali wanadamu!
Ngoja ni kwambie, dhambi humwotea mtu(humvizia) tena humtamani mtu! Dhambi sio tendo bali ni roho iliyokamili, leo kataa kutamanishwa na dhambi, kata kuvutwa na dhambi utafute mti wa uzima uwe hai leo, kwa jina la Yesu.
Kuna mtu dhambi inewahi kumeotea (kumvizia)
"Bwana akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana?
Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.'"
(Mwanzo 4:6-7)
Kuna mtu kila ukiamka unawaza uzinzi, kila ukiamka unawaza pombe, kila ukiamka unawaza ugomvi, unapaswa kujua huo ni mti unaokutamanisha! Unapaswa ukatae kufanya dhambi!
Kwa hiyo mti wa ujuzi wa mema na mabaya ulikuwa unatamanisha!
Unaweza kuwa upo kwenye bustani ya Mungu sasa hivi lakini unaangalia nje na kuona mti unaokutamanisha, unaona afadhali amabao hawajaokoka wanaoa hadi wake watano na michepuko juu!
Kweli dada umeolewa na mumeo lakini ndio hivyo hujatulia kwenye ndoa yako, upo ndani ya wokovu lakini unatamani kuzini, unawaza wanaume uliokuwa nao zamani! Hapo ni dhambi inakuotea ! Hapo ni mauti inakuita! Kaa ndani ya Yesu utakuwa salama anasema "Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu."
(Yohana 15:4)
Kwa hiyo kaa ndani Yesu! Usitoke nje ya wokovu!
Ni kweli kule nje ni walevi wa pombe
Ni kweli kule nje wanashea mabwana, lakini ngoja ni kwambie kule kuna mauti ila wewe upo uzimani.
Kwa hiyo mti wa Uzima ni Yesu!
Yesu ndiye mti wa uzima!
Kaa ndani ya Yesu uwe mzima kwa jina la Yesu.
Kwa hiyo kulikuwa na miti miwili pale Edeni
Mmoja ulikiliwa unampa mtu uzima na mwingine mtu akila anapata mauti!
Sasa baada ya Adamu kumkosea Mungu , mauti ikawa ndani yao, wakaondolewa kwenye bustani hiyo, na mti wa uzima ukalindwa wasije wakala wakishi tena milele!
Ngoja ni kwambie waliookoka wana maisha ya milele!
Bali wasiomwamini Yesu ni wafu wangali wanaishi!
Yaani mwilini ni wazima lakini roho zao ni mfu mbele za Mungu!
Yaani wakifa hawana uzima wa milele!
Kumbuka kuna vifo viwili! Kifo cha kimwili na kifo cha kiroho!
Kifo cha kiroho ni mtu yule wa ndani yaani roho yake kutupwa katika moto wa Jehanamu! Hiyo ndiyo mauti ya pili!
Mtu akimwamini Yesu, huyo ana uzima wa milele!
Kwa hiyo Mungu akauondoa mti wa uzima machoni pao wasije wakala wakaishi milele!
"Bwana Mungu akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele; kwa hiyo Bwana Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa. Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima."
(Mwanzo 3:22-24)
Ahaa Kumbe kuna makerubi wanaolinda njia ielekeayo uzimani!
Ahaa kumbe njia ya wokovu ni ngumu, kuna makerubi kabisa wanaomzuia mtu asimpokee Yesu, wanaomzuia mtu asiokoke yaani hata ukihubiriwa haukubaliki kumbe kuna makerubi wanaokutia uzito usiifuate njia ya uzima ambayo ni Yesu!
Injili imehubiriwa sana lakini makerubi ya uzinzi yamewafunika wasiione njia ya uzima! Njia ya uzima ni nyembamba sana! Watu hawataki kuokoka , kwa sababu kuna makerubi ya ulevi yamewafunika! Watu hawataki kuokoka kwa sababu kuna makerubi ya fasheni za kuzimu yamewafunika unashangaa jumapili kanisani wanawake karibu wote wamevaa suruali ,na wengine vimini na wengine blauzi za migongo wazi na wengine ndiyo kabisa shetani mzima mzima wanamtangaza!
Leo kwa jina la Yesu Kristo ninapasuapasua makerubi hayo yakwachie uwe huru kwa jina la Yesu!
Sasa kuna mtu mmoja amewahi kuwatuma makerubi wamzuie mtu asiamini injili na kumpokea Yesu nyakati za mtume Paulo.
"Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu; mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu. Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani.Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho,akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka?
Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza.
Ndipo yule liwali, alipoyaona yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana."
(Matendo 13:6-12)
Yawezekana anayekuzuia kuokoka ni baba yako, yawezekana anayekuzuia kuokoka ni mume wako, unapaswa kujua ndani yake kuna kerubi anayekuzuia!
Leo pokea nguvu ya kuendelea na wokovu kwa jina la Yesu!
Fuata njia ya uzima kwa jina la Yesu!
Kwa hiyo Mungu akauondoa mti wa uzima!
"Yeye ni mti wa uzima kwao wamshikao sana; Ana heri kila mtu ashikamanaye naye."
(Mithali 3:18)
Kwa hiyo Ukimfuata Yesu unakuwa na uzima!
Yesu ndiye huo mti wa uzima wa milele!
Ninaomba katika jina la Yesu, neema ya Mungu iwe juu yako utambue kuwa Yesu Kristo ndio hiyo njia ya uzima! Ndiyo huo mti wa uzima!
Uzima katika afya, uzima katika kazi, uzima kwenye biashara yako!
Unapaswa kumruhusu Yesu atawale.
" Mazao ya mwenye haki ni mti wa uzima; Na mwenye hekima huvuta roho za watu."
(Mithali 11:30)
Ahaa kumbe wenye haki wanetokana na mti wa uzima ambaye ni Yesu!
Kwa hiyo wenye haki matu yao ni uzima! Watu wanaomwamini Yesu matunda ya vinywa vyao huleta uzima!
Tukisema "uwe mzima unakuwa mzima kwa jina la Yesu! Maana asili yao ni mti wa uzima!
"Kilichotarajiwa kikikawia kuja, moyo huugua. Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima."
(Mithali 13:12)
Uliyetamani kupata mtoto pokea mtoto kwa jina la Yesu! Uliyetamani kuwa mzima uwe mzima kwa jina la Yesu!
Mti wa uzima ukadhihirike kwenye maisha yako kwa jina la Yesu.
"Ulimi safi ni mti wa uzima; Bali ukorofi wa ulimi huvunja moyo."
(Mithali 15:4)
Naomba katika jina la Yesu, kinywa chako kitamke kilichochema kwa jina la Yesu!
Tamko uzima kwenye maisha yako, itakuwa hivyo kwa jina la Yesu!
"Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya Mungu."
(Ufunuo 2:7)
Kwa hiyo unatakiwa kushinda majaribu, uishinde dhambi , ni kwa kumpokea Yesu tu na sio vinginevyo maana Yeye ndiye anaye kushindia ! Ni yeye atakayekuongoza usifanye dhambi!
Hakika utakula matunda yake!
"katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa.
(Ufunuo 22:2)
Kwa hiyo tunajifunza Yesu ndio huo mti wa uzima na matunda aina kumi na mbili ni wale mitume 12,
Kwa hiyo tunaona Yesu ametuponya! Hatukustahili lakini injili ikatufikia tukaamini na sisi tukaponywa katika Neno la Kristo.
"Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake. Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya."
(Ufunuo 22:14-15)
Kwa hiyo kufua nguo ni kutubu dhambi, wewe uliyeokoka umefua nguo tayari, usiangalie nje ya wokovu kuna hao wazinzi nk.
Mungu awabariki sana.
Usisahau ku subscribe YouTube channel yetu ya BinagoTv
Post a Comment