AMKA NA BWANA LEO 10/01/2022

KESHA LA ASUBUHI 
JUMATATU, JANUARI 10 2022

OMBA KWA KUJISALIMISHA KWA MAPENZI YA MUNGU 

Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu. Luka 21:36.

▶️ Mwombe Baba yako wa mbinguni mara kwa mara. Kadiri unavyoshiriki mara kwa mara katika maombi, ndivyo roho yako itakavyovutwa katika ukaribu wa utakatifu wa Mungu. Roho Mtakatifu atafanya maombezi kwa mwombaji wa dhati kwa kuugua ambako hakuwezi kutamkwa, na moyo utalainishwa na kutiishwa kwa upendo wa Mungu. Mawingu na vivuli ambavyo Shetani huvirusha juu ya roho vitaondoshwa kwa miale ing'aayo ya Jua la Haki, vyumba vya akili na moyo vitaangazwa kwa nuru ya mbinguni.

▶️ Lakini, usikatishwe tamaa ikiwa maombi yako hayaonekani kupata jibu la haraka. Bwana anaona kuwa maombi mara nyingi huchanganywa na mambo ya kidunia. Watu huombea kile ambacho kitaridhisha tamaa za ubinafsi wao, na Bwana hatimizi maombi yao kwa njia wanayoitarajia. Huwa anawapitisha katika mitihani na majaribu, akiwanyenyekesha kupitia fedheha, hadi pale watakapoona kwa uwazi zaidi yale yaliyo mahitaji yao. Yeye hawapatii watoto wake vitu vile vitakavyoridhisha tamaa duni, na ambavyo vitaleta madhara kwa mawakala wa kibinadamu, na kuwafanya washindwe kumpa Mungu heshima. Mungu hawapatii wanaume na wanawake vile vitakavyokidhi matakwa yao, na kufanya kazi tu kwa ajili ya kujikweza nafsi. Tunapokuwa tukimwendea Mungu, sharti tuwe wanyenyekevu na wenye mioyo iliyopondeka, tukiweka kila kitu katika mapenzi Yake matakatifu.

🔘 Katika bustani ya Gethsemani, Kristo alimwomba Baba Yake, akisema, "Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke.' Kikombe alichoomba kiondolewe kutoka Kwake, ambacho kilionekana kichungu sana rohoni Mwake, kilikuwa ni kikombe cha utengano na Mungu katika matokeo ya dhambi ya ulimwengu. Yeye ambaye hakuwa na hatia kabisa na wala hakustahili kulaumiwa akawa kama mwenye hatia mbele za Mungu, ili kwamba hatia isamehewe na kusimama bila hatia mbele za Mungu. Wakati alipothibitishiwa kuwa ulimwengu unaweza kuokolewa sio kwa njia nyingine zaidi ya kupitia kwa kafara Yake mwenyewe, Alisema, "Walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe." Roho ya unyenyekevu ambayo Kristo aliidhihirisha katika kutoa ombi Lake mbele za Mungu ndiyo roho ambayo inakubalika kwa Mungu. Hebu roho na ihisi hitaji lake, kutokuwa na msaada kwake, kutokuwa na kitu kwake, hebu nguvu zake zote ziletwe kwake kwa shauku ya dhati ya msaada, na kisha msaada utakuja.
MWENYEZI MUNGU AKUBARIKI SANA

No comments