AMKA NA BWANA LEO 03/12/2021

IJUMAA, DEC 3 2021

*KUSHUKURU KILA WAKATI*

_Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu. Yohana 14:18._

📖 Japokuwa sikupata usingizi wa kutosha usiku uliopita, amani yangu ilikuwa kama mto. Upendo wa Yesu unakua moyoni mwangu, na ninampenda, na moyo wangu unabubujikwa furaha na shukurani. Thamani ya ukweli wa Kimungu inajieleza kwa uwazi na nguvu katika akili zangu kiasi kwamba ninatamani kuuwasilisha kwa wote ambao naweza kuwafikia ili kuwafariji, na kuwapa shime kwa faraja ambayo mimi mwenyewe nafarijika kwayo. Sina hisia zozote zile za kusononeka. Mitazamo na mawazo mazuri vinajileta kwangu kama dhahabu safi, na moyo wangu unaburudika na ninahisi nguvu rohoni ambayo inaonekana kuwa na shauku ya kujitokeza na kujieleza.

📖 Katika kusoma Maandiko, nuru inaonekana kung'aa kwenye kila herufi-sentensi zinaonekana kuwa mpya na muhimu-na moyo wangu uko katika hali ya upatanifu na mwili wote. Ninashukuru kila wakati, hata wakati ninapokuwa macho usiku kwa kukosa usingizi.

📖 Ninajua katika uzoefu wangu wa kila siku kuwa Roho Mtakatifu yupo ninaposoma Neno Lake, akipanda ukweli moyoni mwangu, ili uonekane katika maisha na tabia kwa wengine. Roho wa Mungu huuchukua ukweli kutoka katika kurasa takatifu, mahali ambapo Yeye Mwenyewe aliuweka, na kunatisha rohoni. Furaha takatifu, tumaini na faraja vinaweza kuwa vyetu ili kuwapa wengine.

📖 Nilihudhuria mkutano wa mchana [mahali panapoitwa Ballarat, N.S.W., Australia], na kulikuwa na mahudhurio makubwa zaidi ya watu waliokuja kusikiliza neno la Mungu kuliko nilivyotarajia. Nilihubiri kutoka Yohana 14:15-24. Bwana alinipa maneno ya kuwaambia watu ili kuwapa uhakikisho wa thamani ambao Kristo anawapatia wote wanaomjua na kuzitii amri zake. Yesu anataka ushahidi wa upendo wao Kwake. "Mkinipenda, mtazishika amri zangu" (Yohana 14:15). Kama isingewezekana kuzitunza amri Zake, kwa nini atuambie maneno kama haya? Sasa aya ifuatayo inatufungulia hazina ya maarifa. "Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele” (Aya ya 16)....

🔘 *Je, ahadi hii si ya hakika? Je, maneno yaliyotoka katika midomo ya Mwana pekee wa Mungu yanaweza kuwa ya hakika na chanya zaidi ya hapo?*
MUNGU AKUBARIKI SANA

No comments