DAVID KAFULILA ATOA SIKU 5 WAKULIMA SIMIYU KUONDOA ASALIA

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila, ametoa siku tano kuanzia leo, wakulima wote wa zao la pamba mkoani humo ambao bado hawajaondoa masalia kwenye mashamba yao kuhakikisha wanafanya hivyo mara moja kabla ya Ijumaa ya wiki hii.

Kafulila amesema kuwa kuondoa masalia kwenye shamba kwa mkulima wa zao la pamba ni sheria wala siyo hiari na kusisitiza kuwa hadi kufikia siku hiyo kila mkulima wa zao hilo anatakiwa kuwa ametekeleza agizo hilo la kisheria.

Amesema kuwa sheria inawataka wakulima wa pamba kila mwaka ifikapo Septemba 15, kuondoa masalia na magugu yote kwenye mashamba yao na mkulima atakayekaidi anatakiwa kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria hiyo.

Kwa mujibu wa Sheria Namba 2 ya Tasnia ya Pamba ya Mwaka 2001 kifungu cha 14 kikisomwa kwa pamoja Kanuni ya Tasnia ya pamba ya Mwaka 2011 Kanuni Namba 14, mkulima atakayetenda kosa la kushindwa kuondoa mabaki ya miti ya pamba atahukumiwa kifungo sio chini ya miezi 3 au faini ya sio chini ya 100,000 au vyote kwa pamoja.

No comments