(UNWTO) LAAHIDI KUSHIRIKIANA NA SERIKALI YA TANZANIA

Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii (UNWTO) limeahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuweka mikakati bora ya kuwajengea uwezo  watu waliopo katika sekta ya utalii.

Hatua hiyo inakuja kufuatia hali mbaya inayoikumba sekta ya Utalii nchini na Duniani kwa ujumla kufuatia janga la virusi vya UVIKO 19.

Ambapo pia ikikadiriwa kuwa, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imepata hasara ya Dola 4.8 bilioni za Marekani (Zaidi ya Sh Tirioni 11) kwenye sekta ya utalii kutokana na janga hilo la  UVIKO 19 huku watu milioni 21 wakikosa ajira.

Akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro, Katibu Mkuu wa UNWTO, Zurab Pololkashvili amesema mafunzo hayo yatakayotolewa kwa Wadau wa Utalii yatalenga kuwajengea uwezo Wadau hao katika kujiimarisha na kuendana na janga la UVIKO 19 katika kuendesha shughuli za utalii nchini.

Amesema mafunzo hayo pia yatawalenga watu mbalimbali wenye nia ya kutaka kuingia katika sekta ya utalii nchini ilikutengeneza ajira nyingi kupitia utalii.

Ujumbe wa Tanzania unahudhuria mkutano huo ulioandaliwa na Shirika la UNWTO wa 64 wa Kanda ya Africa ukiongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro unaofanyika kwa muda wa siku nne  katika Kisiwa cha Sal kilichopo  nchini Cape Verde.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo amemueleza Waziri Dkt. Ndumbaro kuwa UNWTO  iko mbioni kuandaa Kalenda  ya mwaka ya UNWTO  ambapo Tanzania nayo itakuwemo katika orodha hiyo kuendana na matukio yatakavyopangwa katika mkutano huo.

"Moja ya kipaumbele cha UNWTO kwa sasa ni kuitangaza Tanzania na Africa kwa ujumla.

Hii pia ni pamoja na kujengea uwezo wadau wa Utalii katika kujiimarisha na kuendana na jangaa UVIKO 19 katika kuendesha shughuli za Utalii Tanzania". Alisema Katibu Mkuu huyo wa UNWTO, Bw. Zurabu Pololkashvili.

Kwa upande wake, Waziri Dkt. Ndumbaro akizungumza katika kikao hicho cha ana kwa ana na Katibu Mkuu huyo, amesema mafunzo hayo yatatoa matumaini kwa Wadau wa Utalii nchini baada ya ugonjwa wa UVIKO 19 kuwatikisa.

No comments