TUHUMA ZA WIZI WA MABATI KILOSA

"Itakumbukwa hivi karibuni iliripotiwa tukio la upotevu wa mabati katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa. Tuhuma hizo zilimhusisha Bw. Asajile Lucas Mwambambale ambaye hapo awali alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kabla ya kuhamishiwa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo"

"Tarehe 09.09.2021 Ofisi ya Rais-TAMISEMI ilipokea taarifa ya maandishi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ikibainisha kuwa kuna upotevu wa mabati 1,172 uliotokea tarehe 17 Agosti, 2021 kwenye Bohari ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa"

"Aidha, taarifa hiyo imeweka wazi kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama imefanikisha kupatikana kwa mabatihayo na yameshapelekwa kwenye maeneo husika na ujenzi wa madarasa unaendelea"

"Halikadhalika Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro alishamwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilosa kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wanne waliochini yake waliohusika na upotevu huo"

"Kufuatia taarifa hiyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Ummy Mwalimu amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo Bw. Asajile Lucas Mwambambale ili kwenda kujibu tuhuma zinazomkabili katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa na pia amemuagiza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - TAMISEMI kupeleka timu huru ya kuchunguza kwa kina suala la aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo"

"Aidha Mhe. Ummy amewakumbusha watumishi wote wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kufanya kazi kwa weledi, kuwa waadilifu na makini katika utendaji kazi wao wa kila siku."---- Ofisi ya Rais-TAMISEMI

No comments