HASSAN MWAKINYO APANDA HADI NAFASI YA 13 DUNIANI
Mwakinyo amepanda kwenye viwango vya ubora baada ya kumtwanga Julius Indongo kutoka Namibia kwenye usiku wa Mabingwa wa Ulingo siku ya Ijumaa Septemba 3 katika ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.
Katika pambano hilo la raundi 12, Mwakinyo alifanikiwa kuibuka na ushindi wa KO kunako raundi ya 4 tu ya mchezo baada ya kumtwanga makonde mfululizo bingwa huyo wa zamani wa mikanda ya WBO na WBC.
Taarifa kutoka BoxRec ambao ni mtandao maarufu kwa rekodi za mchezo wa ngumi duniani, Mwakinyo anaendelea kushikilia nafasi ya kwanza nchini Tanzania na barani Afrika katika uzito wa Super Welter huku akiwa ndiye bondia pekee kutoka barani Afrika mwenye nyota nne.
Mwakinyo mzaliwa wa Makorora jijini Tanga, alifanikiwa kubeba mkanda wa ABU tarehe 28 Mei mwaka huu alipomtwanga muangola, Anthony Maiala na kisha kuutetea Septemba 3 kwenye usiku wa mabingwa wa Ulingo.
Kwa sasa, ni mabondia 12 pekee duniani wa uzito wa Super Welter ambao wapo mbele ya Mwakinyo kwenye viwango vya ubora ambao ni Jarmell Charlo (USA), Brian Carlos Castano (Argentina), Tim Tszyu (Australia), Magomed Kurbanov (Urusi), Erickson Lubin (USA), Liam Smith (USA), Brandon Adams (USA), Jack Culcay (Ujerumani). Carlos Adames (Dominican Republic), Jeff Horn (Australia), Terrell Gausha (USA) na Sergio Garcia (Hispania)
Hizi ni taarifa njema kwa mchezo wa ngumi Tanzania ikiwa ni mara ya kwanza kwa bondia kutoka nchini kufika kwenye nafasi hiyo duniani. Mafanikio haya ya Hassan yakawe ni hamasa kwa mabondia wengine nchini kufukuzia ndoto zao.
Post a Comment