AMKA NA BWANA LEO 5/09/2021

*KESHA LA ASUBUHI.*

Jumapili, 05/09/ 2021.

*MWONGOZO WETU KATIKA KWELI YOTE.*

*Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, Ili akae nanyi hata milele.* Yohana 14:16.

▶️ Kristo alitangaza kwamba, baada ya kupaa kwake, Angetuma kwa kanisa Lake, kama zawadi yake kuu kabisa, Mfariji, ambaye angechukua nafasi Yake. Mfariji huyo ni Roho Mtakatifu ---- nafsi ya maisha Yake, ufanisi wa kanisa Lake, nuru na uhai wa ulimwengu. Kwa Roho wake, Kristo anapeleka mvuto wa kupatanisha na nguvu ya kuondoa dhambi. 

▶️ Mungu ameniagiza kukuambia wewe pamoja na watu wake wote mpate kuwa waangalifu sana msije mkapinga utendaji wa Roho Mtakatifu ---- Mfariji yule ambaye Kristo anamtuma. Ogopa kuchukua hatua ya kwanza ya kiburi cha upinzani. Kristo aliposema na wanafunzi Wake kuhusu Roho Mtakatifu, Alitaka kuinua mawazo yao na kupanua matarajio yao ya kuelewa wazo la juu kabisa la ubora. Hebu na tujitahidi kuelewa maneno Yake. Hebu na tujitahidi kutambua vyema thamani ya karama ya ajabu ambayo ametupatia. Hebu tutafute utimilifu wa Roho Mtakatifu ....

▶️ Sioni njia nyingine kwetu isipokuwa kuyatii maneno ya Kristo, "Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate" (Mathayo 16:24). Maneno haya ni lazima tuyatii ikiwa tunataka kuupata uzima wa milele. Mkuu wa Mbinguni alikuja hapa ulimwenguni kutufundisha somo hili kwa maisha ya kujinyima kila wakati. Je! Hatuyatii mafundisho yake?

▶️ Ili kuokolewa, ni lazima tuwe na uzoefu kamili na mtimilifu katika mambo ya Mungu. Upatanisho wa dhambi umefanywa kwa karama ya Mwana wa Mungu asiye na kikomo ....

▶️ Kumleta mwenye dhambi kwa Kristo ni kazi ya Mfariji, Roho Mtakatifu. Mwokozi ni mfano wa kiungu, upeo wa utakatifu, na Yeye hutengeneza roho upya. Tumebahatika kupokea kutoka Kwa Kristo uzuri wote unaohitajika Kwa ajili ya ukamilifu wa tabia. Lakini ili tuweze kuupata ubora huu, ni lazima tuonyeshe kujinyima zaidi, kujitolea zaidi. 

▶️ *Kristo ametufanyia kila njia ya sisi kuwa watoto wa Mungu. Ndio, moyo wangu unasema, Sifu Jina lake takatifu ili kwa utimilifu wake tuweze kupokea neema baada ya neema. Hebu na tujitahidi, kwa kulipokea neno Lake, kufikia kiwango cha juu cha ukamilifu. Tuko Salama pale tu tunapotafuta sifa zile zinazotufanya sisi kuwa watoto wa Mungu, wamiliki wa ubora uliotakaswa.*

*MUNGU ATUBARIKI SOTE.*

.
Follow us @binagotv👇🏾

No comments