AMKA NA BWANA LEO 08/09/2021

*KESHA LA ASUBUHI*

Jumatano, Septemba 08, 2021

*ILI IMANI YAKO ISITINDIKE*

*Katika Bwana nafsi yangu itajisifu, Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.* Zaburi 34:2

📚 Pale, unapokuwa unatenda kazi kwa ajili ya wokovu wa roho, watenda dhambi wanasadikishwa kuhusu dhambi zao nawe una ushahidi kwamba Kristo amewahurumia, kwamba matumaini mapya yanachipuka mioyoni mwao, sio sahihi kusema, “Tulimwombea, naye akatoa moyo wake kwa Mungu na ameokoka.” Hii inapotosha. Ni haki yao kusema, kwa umakini, kwa dhati, kwa furaha, “Ninaamini kwamba Yesu Kristo amenisamehe dhambi zangu.” Tia moyo kila roho kuwa na tumaini na imani, lakini kamwe…. usiseme kuhusu mtu yeyote, “Ameokoka.”….
 
📚 Wema, wenye uvumilivu, unapaswa kutendwa kwa wale wanaokosea, ili kumrejesha kondoo anayetangatanga. Tunao mfano wa hili katika jinsi Kristo alivyomtendea Petro ambaye alimkana Bwana wake kwa kulaani na kuapa. Petro alijidhania kuwa mwenye nguvu. Alisema, “Bwana, kwa nini mimi nisiweze kukufuata sasa? Mimi nitautoa uhai wangu kwa ajili yako.” (Yohana 13:37). Lakini Yesu akamjibu, “Amini, nakuambia wewe, leo, usiku huu, kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu.” (Marko 14:30). Lakini Petro “akazidi sana kusema, Ijaponipasa kufa nawe, hata hivyo sitakukana kamwe.” (aya ya 31).
 
📚 Sio busara kujivuna. Petro alianguka kwa sababu hakujua udhaifu wake mwenyewe…. Bwana alikuwa amemwambia Petro, “Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.”(Luka 22:31, 32).

🔘 *Iwapo Shetani angeachwa kutenda apendavyo, kusingelikuwa na tumaini lolote kwa Petro. Angelifanya uharibifu kamili wa imani. Kama Petro kwa bidii na kwa unyenyekevu angetafuta msaada wa kiungu, kama angekuwa akichunguza moyo wake mwenyewe kwa siri, asingepeperushwa alipojaribiwa. Shetani hawezi kumshinda mwanafunzi mnyenyekevu wa Kristo, yeye ambaye hutembea kwa maombi mbele za Bwana. “Adui atakapokuja kama mkondo wa mto ufurikao, (Roho wa Bwana atainua bendera)” kwa ajili yake dhidi ya adui (Isaya 59:19). Kristo anaingilia kati Yeye mwenyewe kama kinga, kimbilio, na yule mwovu hawezi kumshinda.*

*MUNGU AKUBARIKI SANA*

No comments