DOZI 1,008,400 ZA CHANJO ZASAMBAZWA NCHI NZIMA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi, amesema Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea
kuratibu utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 (COVID-19) kupitia vituo vya kutolea huduma za Afya vya umma na binafsi vilivyoidhinishwa hapa nchini. 

Hadi kufikia tarehe 14.08.2021 Prof. Makubi amesema jumla ya dozi 1,008,400 za chanjo ya UVIKO-19 zilikuwa zimesambazwa katika mikoa yote 26 na chanjo imekuwa ikitolewa katika vituo vya kutolea huduma zaidi ya 550 kwa Tanzania bara.

Tathimini ya zoezi la utoaji chanjo tangu Mikoa yote izindue tarehe 04/08/2021, Prof. Makubi amesema inaonesha mpaka kufikia tarehe 14.08.202, jumla ya walengwa 207,391 wamepatiwa chanjo, kati ya hawa walengwa, 121,002 ni wanaume (58.3%) na 86,389 (41.7%) ni wanawake.

"----->Katika vituo vyote/Hospitali, natoa maelekezo kwa watoa huduma wote, kutumia
dakika chache kutoa elimu ya umuhimu wa chanjo kwa kila mteja atakaye mhudumiwa kwa magonjwa mengine ili kumpa nafasi ya uelewa na baadae yeye kuchukua maamuzi sahihi juu ya chanjo, aidha pasiwepo na sababu yoyote ya
Wananchi waliofika vituoni kukosa au kukataliwa kupata huduma ya chanjo"----- MAKUBI

Mwisho, Wizara pamoja na kupongeza mamlaka za Mikoa, Wilaya na Mitaa kwa kuhamasisha zoezi la chanjo, ametaka pia na juhudi zaidi za kuongeza kasi katika maeneo ya pembezoni ya miji, mitaa na vijijni.

Amewaasa Wananchi waendelee kuchukua tahadhari zote za kinga dhidi ya UVIKO-19 kwa kunawa mikono na maji tiririka/kutumia vipukusi, kuvaa barakoa katika maeneo hatarishi, kuepuka misongamano isiyokuwa ya lazima na kufanya mazoezi kila mara.

No comments