RAIS SAMIA AWAONGOZA VIONGOZI KUMUAGA MFUGALE
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 02 Julai, 2021 amewaongoza viongozi mbalimbali na waombolezaji kuaga mwili wa aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale.
Shughuli za kuaga mwili wa Mhandisi Mfugale zimefanyika katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein Katanga, Katibu Mkuu Kiongozi-Zanzibar Mhandisi Zena Said pamoja na viongozi
wengine wa Taasisi za Umma na Binafsi.
Mhe. Rais Samia amesema kifo cha Mhandisi Mfugale kimeacha simanzi na pengo kubwa kwa familia, Serikali na Taifa kwa ujumla.
Amesema Serikali imepoteza mtumishi na kiongozi mwadilifu, makini, shupavu na mchapakazi hodari. Taifa limepoteza Mhandisi mahiri na mzalendo wa kweli ambaye daima alikuwa tayari kuitumikia nchi kwa moyo wake wote.
Mhe. Rais Samia amesema Mhandisi Mfugale ameacha alama kubwa kwa nchi kwa kuwa amekuwa mtumishi wa umma kwa takriban miaka
45, tangu mwaka 1977 ambapo ameongoza TANROADS kwa takriban miaka 12 tangu mwaka 2009.
Katika kipindi hicho Mhandisi Mfugale ametoa mchango mkubwa kwa nchi hususan katika sekta ya miundombinu ya barabara na madaraja.
Aidha, Mhe. Rais Samia amesema Mhandisi Mfugale atakumbukwa kwa kubuni na kusimamia ujenzi wa Daraja la Umoja (Mtambaswala)
linalounganisha Tanzania na Msumbiji, Daraja la Nyerere (Kigamboni), Daraja la Mkapa katika Mto Rufiji, Daraja la Kikwete katika Mto Malagarasi, Daraja la Magufuli katika Mto Kilombero,
Daraja la Mfugale TAZARA), Daraja la Kijazi Ubungo), Daraja la Tanzanite (Selander), Daraja la Kigongo - Busisi (JPM, na Miradi mingi ya kimakakati.
Mhe. Rais Samia amesema kutokana na mchango mkubwa alioutoa Mhandisi Mfugale kwa Taifa, kila mmoja wetu anapaswa kutumiabfursa aliyopewa kuacha alama ili nchi ipate maendeleo kwa haraka.
Mhandisi Mfugale alifariki dunia Juni 29, 2021 katika hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma.
Post a Comment