MSIGWA;HATUJALAZIMISHA MTU, CHANJO NI HIARI YAKO
Msemaji Mkuu wa Serikali Mhe. Gerson Msigwa amesema Serikali haijatoa maelekezo ya kuwalazimisha watumishi wa umma kupokea chanjo dhidi ya ugonjwa wa Korona (Uviko-19) kama ambavyo imezushwa na wahalifu kupitia mitandao ya kijamii.
Amewataka wananchi wakiwemo watumishi wa umma kupuuza uzushi huo na kuendelea kupokea taarifa rasmi kutoka Serikalini kupitia kwa viongozi na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu juu hafua mbalimbali za kujikinga na Uviko-19.
"Msimamo wa Serikali ni kuwa utoaji wa chanjo ya Uviko-19 unafanyika kwa hiari ya mtu yeyote
atakayekuwa tayari kupokea chanjo hiyo"
"Na kwa kuanzia makundi yatakayopewa kupaumbele ni watumishi wa afya (Madaktari na Wauguzi), Watu wenye magonjwa sugu, watu wenye umri wa zaidi ya miaka 50 na Askari waliopo katika vyombo vya ulinzi na usalama"
Serikali inawataka wanaofanya uhalifu huu wa kuzusha, kufanya uchochezi na kuwatisha
wananchi kuacha mara moja kwa kuwa ni makosa kisheria.
"Wananchi wote endeleeni kuchukua tahadhari kama zinavyoelekezwa na wataalamu wa afya zikiwemo kunawa mikono mara kwa mara kwa maji yanayotiririka na sabuni, kuvaa barakoa,
kujiepusha na misongamano isiyo ya lazima na kuzingatia umbali usiopungua mita moja kutoka
mtu mmoja hadi mwingine"
"Kwa hivi sasa Serikali inaendelea kukamilisha maandalizi ya kutoa chanjo katika Mikoa 10
itakayoanza kutoa chanjo kwa wananchi na utaratibu utakapokamilisha mtajulishwa."---- GERSON MSIGWA
Post a Comment