KITUO CHA KUPOZA UMEME KUJENGWA KONGWA

Waziri wa Nishat, Dkt.Medard Kalemani amesema Serikali itajenga kituo kikubwa cha kupoza Umeme katika Wilaya ya Kongwa ili kumaliza tatizo la kukatika umeme mara kwa mara na kuboresha upatikanaji wa Umeme katika wilaya hiyo na maeneo jirani.

Dkt. Kalemani alisema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miundombinu ya umeme ikiwa ni pamoja na kutembelea eneo litakalojengwa kituo hicho lililopo katika Kijiji cha Machenje Kata ya Ugogoni Wilayani ya Kongwa mkoani Dodoma,Julai 27,2021.

Katika ziara hiyo, Dkt. Kalemani alisema kuwa tayari eneo la ukubwa wa Hekari 130 limepatikani ambalo litatumika kujenga kituo hicho, kitakachokuwa na uwezo wa kufua umeme wa Kilovolti 220.

Aidha alisema kuwa tayari zaidi ya shilingi milioni 63 zimetengwa kwa ajili ya kuwalipa fidia wakazi wa eneo hilo watakaopisha Ujenzi wa Mradi husika ambao utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 41.2.

Ujenzi wa kituo hicho unatajia kuanza kutekelezwa mapema mwezi Septemba mwaka huu 2021.

“Tuna umeme mwingi sana Mkoa wa Dodoma, lakini kuna changamoto kubwa kukatika umeme na wenye nguvu ndogo katika maeneo yote ya Wilaya ya Kongwa, kwa kipindi cha miaka mingi sana, hii inatokana na umeme huo kusafiri umbali mrefu kutoka kituo cha Zuzu hadi kufika huku takribani kilomita 120 na mzunguko ni takribani Kilomita 2000, suluhisho la kudumu ni ujenzi wa kituo cha kufua umeme ambacho kitamaliza kabisa tatizo hilo na kuwa historia, hasa katika Viwanda, Wafanyabiasha na watumiaji wengine”, alisema Dkt. Kalemani.

Hata hivo alisema kuwa, katika kutatua tatizo la kukatika Umeme mara kwa mara katika maeneo ya Mbande, Kibaigwa, Kongwa, Mpwapwa na Kiteto, ndani ya wiki hii kitafungwa kifaa maalum, kinachojulikana kama AVR ili kuuongeza nguvu ya Umeme katika maeneo hayo.

Dkt. Kalemani alifafanua kuwa kifaa hicho tayari kimeshatoka mkoani Ruvuma kuja Dodoma na kufungwa katika eneo la Mbande.

Sambamba na hilo kazi ya Ujenzi wa Njia ya kusafirisha Umeme wa kV 220 inaendelea kujengwa kutoka Zuzu kupitia Mpunguzi hadi kufika wilayani humo ili kupunguza tatizo la kukatika kwa Umeme mara kwa mara katika maeneo tajwa na mengine jirani.

No comments