AMKA NA BWANA LEO 2

IJUMAA, JULAI 2, 2021

*_KESHA LA ASUBUHI, LESONI NA USOMAJI WA BIBLIA KWA MPANGO*

_*KESHA LA ASUBUHI*_

_Ijumaa, Julai 2, 2021_

*SOMO: NINYI NYOTE NI NDUGU*

```Lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi. 1 Petro 5:2, 3```

*✍️Ni nani aliyempa mwanadamu uhai wake? Nani alimpa akili yake? Je, si Mungu? Hebu Mkristo ambaye anamtegemea Mungu kwa kila pumzi anayovuta, asijisikie kuwa na hadhi ya juu kuliko ndugu zake. Hapaswi kuwawekea masharti, kana kwamba amewapa uhai na akili, na kwa hiyo wanawajibika kwake.*

```¶Inajitokeza miongoni mwetu roho ambayo Mungu hatakubali itawale. Kamwe wakristo hawapaswi kujisikia kwamba wao ni mabwana juu ya Urithi wa Mungu. Haipaswi kuwapo miongoni mwa Wakristo roho ambayo inawafanya wengine kuwa walezi na wengine kuwa wafuasi. Amri za Mungu zinakataza hili. "Baba yenu ni mmoja" (Mathayo 23:8). Hakuna mtu anayepaswa kufikiri kwamba yeye ndiye mmiliki wa akili na vipaji vya ndugu zake. Hapaswi kufikiri kwamba wengine lazima watii amri yake. Anaweza kupotoka, anaweza kufanya makosa, kama ilivyo kwa kila mwanadamu. Hapaswi kujaribu kusimamia mambo kulingana na mawazo yake.

¶Yeye anayesalimu amri kwa roho hii ya kujiinua anajiweka yeye mwenyewe chini ya utawala wa adui. Ikiwa wahudumu wa injili hawataweza kupatana na mawazo na ubunifu wake wote, anageuka kutoka kwao na kusema kinyume nao, akimimina kejeli na uchungu uliomo moyoni mwake juu wachungaji na juu ya huduma.```

*¶Hakuna hata moja ya kazi hii iliyo na kibali cha Mungu. Wakristo wanapaswa kudhihirisha upole wa Kristo, na hili watalifanya ikiwa Kristo anakaa moyoni. Watamtambua Kristo ndani ya ndugu zao. Watapokea ushauri mzuri kwa pamoja. Kama sura za giza za historia ya wanadamu zingelifuatiliwa kulingana na ukweli, ni kiasi gani wangehadaika  wale wanaotumia mamlaka makubwa sana, ambao wanajisikia kuwa wana uwezo wa kusema kwamba wengine watafanya kama wanavyoamuru.*

_✍️Yesu ametupa mfano katika maisha yake ya usafi na utakatifu mkamilifu. Nafsi ililyotukuka kabisa mbinguni, ndiye aliyekuwa tayari zaidi kutumikia. Aliyeheshimiwa mno, alijinyenyekeza kuwahudumia wale ambao muda mfupi kabla ya pale walikuwa wakibishana kuhusu ni nani anapaswa kuwa mkuu  katika ufalme wake. Kutafuta yatupendezayo sisi haidhuru inawaathiri vipi wengine ni uzoefu mgumu sana kuupata._

```LESONI, JULAI 2

JIFUNZE ZAIDI:

¶“Kulingana na mtazamo wa marabi, ukamilifu wa dini ulipaswa kuonekana katika pilikapilika za shughuli wakati wote. Walitegemea mwonekano wa nje ili kuonesha utauwa wao wa kiwango cha juu. Kwa namna hiyo walijitenga nafsi zao na Mungu, na kujijenga wenyewe katika kujitosheleza nafsi. Hatari ya aina ile ile ipo hata leo. Kadri shughuli zinavyozidi na watu wakifanikiwa katika kazi ya Mungu, 

¶kuna hatari ya kutegemea mipango na mbinu za kibinadamu. Kuna kawaida ya kuwa na maombi machache na imani haba pia. Kama ilivyokuwa kwa wanafunzi, tupo hatarini kupoteza mwelekeo wa utegemezi kwa Mungu, na kujaribu kufanya shughuli zetu kuwa mwokozi. Tunahitajika kumtazama Yesu daima, tukitambua kwamba uwezo wake ndio unaoifanya kazi. Huku ikitupasa kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya wokovu wa waliopotea, lazima pia tuwe na muda wa kutafakari, kuomba, na kujifunza neno la Mungu. Kazi tu ambayo imetimilika kwa njia ya maombi mengi, na kwa uthibitisho wa Kristo, ndiyo hatimaye itakayothibitishwa kuwa yenye ufanisi kwa uzuri.” —Ellen G. White, The Desire of Ages, uk. 362.

MASWALI YA KUJADILI:

1. Msongo usiokoma wa kuwa mtawala, kuwepo (kimwili au kwa kukaribia) wakati wote, na kujaribu kutimiza njozi ambazo hazina uhalisia wala hazitoki kwa Mungu vinaweza kuwafanya watu waugue-kihisia, kimwili, na kiroho. Kwa namna gani kanisa lako linaweza kuwa sehemu ya kuwakaribisha waliolemewa, watu waliochoka wakitamani pumziko? 

2. Je, inawezekana kwamba tuna shughuli nyingi mno, hata katika kufanya mambo mazuri kwa ajili ya Mungu? Fikiria kuhusu kisa cha Yesu na wanafunzi wake katika Marko 6:30—32 na kujadili matumizi katika kundi lako la Shule ya Sabato.

3. Mwaka 1899, rekodi ya mwendo ilivunjwa. Mtu kwa hakika alikwenda maili 39.24 kwa saa kwa gari na kusalimika! Leo, bila shaka, magari huenda kasi zaidi ya hapo. Na kasi ya vichakato katika simu zetu za mkononi ni zaidi tarakilishi kubwa ya kizazi kilichopita. Na usafiri wa anga ni wa kasi kuliko ulivyokuwa, na unazidi kuwa wa kasi zaidi. Hoja ni kwamba karibia kila kitu tunachokifanya leo kinafanyika kwa haraka zaidi kuliko ilivyokuwa wakati uliopita, na bado, nini? Bado tunahisi kuharakishwa pasipo pumziko la kutosha. Hilo linapaswa kutuambia nini kuhusu hali ya asili ya mwanadamu na kwa nini Mungu alifanya pumziko liwe muhimu kiasi cha kuwa moja ya amri zake? 

✍️Tafakari juu ya wazo kwamba hata katika Edeni, kabla ya dhambi, pumziko la Sabato lilianzishwa. Kando ya maana ya kushangaza ya kiteolojia ya ukweli huu, hili linapaswa kutuambia nini kuhusu jinsi pumziko lilivyohitajika hata katika ulimwengu mkamilifu, usio na dhambi?```

USOMAJI WA BIBLIA KWA MPANGO

LUKA 20


1. Ikawa siku moja, alipokuwa akiwafundisha watu hekaluni, na kuihubiri habari njema, wakuu wa makuhani na waandishi pamoja na wazee walimtokea ghafula; 

2. wakamwambia, wakisema, Tuambie, unatenda mambo hayo kwa mamlaka gani? Tena, ni nani aliyekupa mamlaka hii? 

3. Akajibu akawaambia, Nami nitawauliza ninyi neno moja; niambieni, 

4. Ubatizo wa Yohana, je! Ulitoka mbinguni au kwa wanadamu? 

5. Wakahojiana wao kwa wao, wakisema, Kama tukisema ulitoka mbinguni, atasema, Basi, mbona hamkumwamini? 

6. Na tukisema ulitoka kwa wanadamu, watu wote watatupiga kwa mawe, kwa kuwa wamemkubali Yohana kuwa ni nabii. 

7. Wakajibu, kwamba, Hatujui ulikotoka. 

8. Yesu akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya. 

9. Akaanza kuwaambia watu mfano huu; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu; akapangisha wakulima, akaenda akakaa katika nchi nyingine muda mrefu. 

10. Na wakati wa mavuno alituma mtumwa kwa wale wakulima ili wampe baadhi ya matunda ya mizabibu; wakulima wakampiga wakamfukuza mikono mitupu. 

11. Akatuma na mtumwa mwingine. Wakampiga huyu naye, wakamwaibisha wakamfukuza mikono mitupu. 

12. Akamtuma na wa tatu; huyu naye wakamtia jeraha, wakamtupa nje. 

13. Basi, bwana wa shamba la mizabibu alisema, Nifanyeje? Nitamtuma mwanangu, mpendwa wangu; yamkini watamheshimu yeye. 

14. Lakini, wale wakulima walipomwona, walishauriana wao kwa wao, wakisema, Huyu ndiye mrithi; haya, na tumwue, ili urithi uwe wetu. 

15. Wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi, bwana wa shamba la mizabibu atawatendeje? 

16. Atakuja na kuwaangamiza wakulima wale, na lile shamba la mizabibu atawapa wengine. Waliposikia hayo walisema, Hasha! Yasitukie haya! 

17. Akawakazia macho akasema, Maana yake nini basi neno hili lililoandikwa, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni? 

18. Kila mtu aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika-vunjika; na ye yote ambaye litamwangukia litamsaga kabisa. 

19. Nao waandishi na wakuu wa makuhani walitafuta kumkamata saa iyo hiyo, wakawaogopa watu, maana walitambua ya kwamba mfano huu amewanenea wao. 

20. Wakamvizia-vizia, wakatuma wapelelezi waliojifanya kuwa watu wa haki, ili wamnase katika maneno yake, wapate kumtia katika enzi na mamlaka ya liwali. 

21. Wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, twajua ya kwamba wasema na kufundisha yaliyo ya haki, wala hujali cheo cha mtu, bali unafundisha njia ya Mungu kwa kweli. 

22. Je! Ni halali tumpe Kaisari kodi, au sivyo? 

23. Lakini yeye alitambua hila yao, akawaambia, 

24. Nionyesheni dinari. Ina sura na anwani ya nani? Wakamjibu, Ya Kaisari. 

25. Akawaambia, Basi, vya Kaisari mpeni Kaisari, na vya Mungu mpeni Mungu. 

26. Wala hawakuweza kumshitaki kwa maneno yake mbele ya watu; wakastaajabia majibu yake, wakanyamaa. 

27. Kisha baadhi ya Masadukayo wakamwendea, wale wasemao ya kwamba hakuna ufufuo, wakamwuliza, 

28. wakisema, Mwalimu, Musa alituandikia ya kuwa, mtu akifiwa na ndugu yake mwenye mke, lakini hana mtoto na amtwae huyu mke, ampatie ndugu yake mzao. 

29. Basi, kulikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa mke, akafa hana mtoto; 

30. na wa pili [akamtwaa yule mke, akafa hana mtoto;] 

31. hata wa tatu akamwoa, na kadhalika wote saba, wakafa, wasiache watoto. 

32. Mwisho akafa yule mke naye. 

33. Basi, katika ufufuo atakuwa mke wa yupi? Maana aliolewa na wote saba. 

34. Yesu akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; 

35. lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi; 

36. wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo. 

37. Lakini, ya kuwa wafu hufufuliwa, hata na Musa alionyesha katika sura ya Kijiti, hapo alipomtaja Bwana kuwa ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. 

38. Naye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa kuwa wote huishi kwake. 

39. Waandishi wengine wakajibu wakamwambia, Mwalimu, umesema vema; 

40. wala hawakuthubutu kumwuliza neno baada ya hayo. 

41. Akawaambia, Wasemaje watu kwamba Kristo ni Mwana wa Daudi? 

42. Maana, Daudi mwenyewe asema katika chuo cha Zaburi, Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, 

43. Hata niwaweke adui zako Kuwa kiti cha kuwekea miguu yako. 

44. Basi Daudi amwita Bwana; amekuwaje mwana wake? 

45. Na watu wote walipokuwa wakimsikiliza, aliwaambia wanafunzi wake, 

46. Jilindeni na waandishi, wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele karamuni. 

47. Wanakula nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu. Hao watapata hukumu iliyo kuu.

*MUNGU AKUBARIKI SANA*

No comments