WAHITIMU 24 wa masomo ya sayansi kutoka vyuo mbalimbali nchini, wamepata ajira kupitia Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Naliendele, kilichopo Mkoani Mtwara.
Kaimu Mkurugenzi wa kituo hicho Dk. Fortunus Kapinga, amesema wahitimu hao ni wale wanaopita kufanya mazoezi ya kazi kwa vitendo (internship) katika kituo hicho.
"Takriban wahitimu 24 wamepata ajira za kudumu ndani na nje ya nchi kupitia kituo chetu hichi," amesema Dk. Kapinga.
Kadhalika, amesema wamekuwa na kawaida ya kupokea wahitimu kutoka vyuo mbalimbali na kuwapa mafunzo kwa vitendo ambayo yamekua yakiwapa uzoefu mkubwa.
"Mara nyingi vyuoni wanafunzi husoma kwa nadharia, lakini hapa kwetu tunawapa mafunzo kwa vitendo maana wanakuwa sehemu ya wafanyakazi wetu, na sisi hapa asilimia kubwa ya wafanyakazi wetu ni watafiti kwa hiyo hapa wanapata uzoefu wa kazi," ameongeza Dk. Kapinga.
Mhitimu wa mafunzi ya Kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), kilichopo Morogoro, Lucy Kitwange, amesema TARI imemjengea uwezo wa kufanya kazi kwa weledi kupitia ujuzi na maarifa aliyoyapata kwa vitendo.
"Ujuzi na uwezo ni kitovu cha soko la ajira kwa sasa" anamalizia Lucy.
Naye Mariam Shomari, mhitimu wa Kilimo na Baiolojia kutoka SUA, anasema mafunzo hayo ya TARI yamemjengea uzoefu wa kazi kwa kujua majukumu ya kazi na uelewa mpana wa vitu alivyovisoma darasani.
0 Comments