Wakulima wa pamba Mkoani Simiyu, wameipongeza serikali kwa kuimarika kwa bei ya zao hilo kutoka sh. 800 kwa kilo, iliyokuwepo mwaka jana, hadi kufikia sh. 1,150 mwaka huu.
Kadhalika, wamepongeza matumizi ya mfumo wa sasa wa kulipwa fedha baada ya kuuza, kuwa ni mzuri tofauti na ule wa awali wa kuwekewa fedha benki au kwenye mitandao.
"Utaratibu wa mwaka huu ni mzuri, tunalipwa fedha taslimu, tofauti na mwaka jana ambapo tulikuwa tukisubiri kuwekewa kwenye akaunti au kwenye simu," amesema Ndulu Buhulu, mkulima wa pamba kutoka Nkololo, Bariadi .
Akizungumzia hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga, alisema kuimarika huko kwa bei kumetokana na juhudi za serikali katika kuhakikisha wakulima wananufaika.
DC huyo alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti wakati akitembelea maeneo ya kuuzia pamba, huku akiwataka wanunuzi kuepuka kununua pamba ya magendo.
Aliongeza kuwa ambapo hatasita kutaifisha pamba ya mnunuzi ambaye atawanyanyasa wakulima kwa kuwalaghai na malipo kidogo .
"Mwaka jana nyie ni mashuhuda, wanunuzi wote waliofanya biashara za magendo niliwakamata nikataifisha pamba na fedha zilizopatikana baada ya kuuza pamba ya magendo zilifanya shughuli za kimaendeleo kwa manufaa ya wananchi" amesema Kiswaga.
Naye Ofisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya Bariadi, Mulokozi Kato, amesema makisio ya halmashauri kwa msimu huu (2021/2022), ni kukusanya kilo milioni 24 za pamba huku akiwatahadharisha wakulima kutoichafua pamba yao.
0 Comments