Katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Mkoa wa Arusha, Yasmin Bachu, amekabidhi msaada wa taulo za kike, mafuta ya kupaka na sabuni kwa Shule ya Sekondari Mwandeti iliyopo wilayani Arumeru, mkoani Arusha.
Akikabidhi msaada huo, Bachu amewataka wanafunzi wa shule hiyo, kusoma kwa bidii kwa malengo ya kufaulu na kuwa viongozi wa taifa la kesho, kwa sababu serikali imeweka mazingira rafiki ya wanafunzi kusoma katika shule hiyo.
Mwanafunzi Amina Ally, akishukuru kwa niaba ya wenzake, alisema msaada huo una umuhimu mkubwa kwa watoto wa kike na kumuahidi mwenyekiti huyo kufanya vizuri kwenye mitihani yao ya kuhitimu kidato cha nne na cha pili.
Pia Amina ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwaagiza viongozi wa kila mkoa nchini kuwa na shule ya sayasi ya wasichana ili kuwajengea uwezo kusoma masomo ya sayansi.
Naye Makamu Mkuu wa shule hiyo, Lekara Saket, aliishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutoa kiasi cha sh. milioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili ambayo yatachukua wanafunzi themanini kila bweni.
0 Comments