Advertisement

Responsive Advertisement

RAIS SAMIA ATANGAZA SIKU 7 ZA MAOMBOLEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametangaza siku 7 za Maombolezo ya Kitaifa, kufuatia kifi cha Rais wa kwanza wa Zambia, Dkt. Kenneth David Kaunda, kilichotokea jana tarehe 17 Juni, 2021 mjini Lusaka Zambia. 

Katika kipindi hicho cha maombolezo, bendera zote zitapepea nusu mlingoti. 

Aidha, Mhe. Rais Samia ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Zambia, Mhe. Edgar Chagwa Lungu, familia ya marehemu na wananchi
wote wa Zambia kwa kumpoteza kiongozi wao.
Mhe. Rais Samia amemtaja Hayati Dkt. Kaunda kuwa miongoni mwa viongozi mahiri na jasiri kuwahi kutokea barani Afrika, ambapo wakati
wa uhai wake alitoa mchango mkubwa kwenye harakati za ukombozi wa Bara la Afrika kwa kushirikiana na viongozi wengine, akiwemo Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Vilevile, Hayati Dkt. Kaunda alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Tanzania itamkumbuka Hayati Dkt. Kaunda kwa mchango wake katika kukuza uhusiano na ushirikiano kati mataifa yetu mawili, ambao
uliwezesha kutekelezwa kwa miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo Mamlaka ya Reli kati ya Tanzania na Zambia (TAZARA) na Bomba la
Kusafirisha Mafuta (TAZAMA).

Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema Peponi.

Post a Comment

0 Comments