AMKA NA BWANA LEO 20
KESHA LA ASUBUHI
JUMAPILI, JUNI, 20, 2021
SOMO: URITHI WENYE UTUKUFU
Haleluya. Msifuni Mungu katika patakatifu pake; Msifuni katika anga la uweza wake. Msifuni kwa matendo yake makuu; ...Kila mwenye pumzi na amsifu BWANA. Haleluya.
Zaburi 150:1—6.
Jana saa nne kamili tulifika katika eneo hili —East Portland, Oregon. Tulipokuwa njiani kutoka Walla Walla Jumanne asubuhi magari yalisimama, kama yanavyofanya kwa kawaida, dakika ishirini katika Maporomoko ya Multnomah. Karibu watu wote walitoka kwenye magari ili wapande kwenye mwinuko wa juu wapate mwonekano mzuri wa uzuri huu wa kushangaza, sehemu nzuri ya kutazama.
Kulikuwa na ngazi zilizojengwa ukingoni, kisha njia nyembamba ya zigizaga, kisha ngazi zaidi za mbao. Hii ilirudiwa mara nyingi hadi tulipofika na kuvuka daraja ambalo liliweka genge kubwa juu ya maporomoko ya kwanza. Maporomoko makubwa yapo juu ya hili na yanaitwa Utaji wa Bibi Harusi (Bridal Veil). Kimo kutoka ambapo maji yanaporomoka ni takriban futi 900. Kadiri maji yanavyoporomoka yanavyobandua mawe, na kutawanya manyunyu yanayopendeza. Ni sehemu inayopendeza kutazama.
Ningefurahi sana kama ningetumia siku nzima katika sehemu hii iliyozungukwa na mazingira ya kupendeza. Lakini tulifurahi kwa dakika chache hizi kutazama mazingira ya asili yanayopendeza, ingawa tulilazimika kutaabika kupanda mlima ili kuweza kutazama, kusimama kwenye daraja kulikuwa ni kwa kusudi hili.
Nilikumbuka maneno ya mtunga Zaburi anapokiita kila chenye pumzi kimsifu Bwana, viumbe hai na visivyo hai viungane katika kibwagizo kimoja cha kusifu na kumshukuru Mungu. Wito wake huo kwa viumbe visivyo na fahamu, visivyofikiria ni kemeo kubwa kwa wale waliobarikiwa kuwa na akili, ikiwa roho zao hazichangamki na midomo yao haitangazi ukuu na utukufu wa Mungu.
“Msifuni, jua na mwezi; Msifuni, nyota zote zenye mwanga.... Msifuni BWANA kutoka nchi, Enyi nyangumi na vilindi vyote. Moto na mvua ya mawe, theluji na mvuke, Upepo wa dhoruba ulitendao neno lake.” (Zaburi 148:3—8). Mawakala wote hawa wa Mungu katika mazingira ya asili wanaitwa kuleta sifa kwake Yeye Aliye juu. Na nani ambaye miongoni mwa viumbe wa Mungu atakuwa kimya wakati kila nyota inapotenda kazi yake, kila upepo unaposafisha dunia, na kila wingu linaloleta giza, kila tone la mvua na kila mwale wa mwanga wa jua, viumbe vyote hivi vinamsifu Mungu anayetawala mbinguni?
—Manuscript 9, Juni 20, 1884,, “Ziara kwenda Maporomoko ya Multnomah.”
Post a Comment