RAIS SAMIA AWEKA MFANO WA MAVAZI KWA WANAWAKE TZ

*TANZANIA: WANAWAKE HUDHURIENI DARASA LA MAVAZI YA STARA KWA RAIS SAMIA.*

_Anaandika Mwl. Paul Gregory : DSM; Tanzania_

Tangu Rais Samia Suluhu Hassan ashike hatamu za uongozi kama Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania mnamo siku ya Ijumaa, 19 Machi 2021 kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa JMT hayati John Pombe Magufuli; watanzania wamekuwa na shauku kubwa ya kuona mambo mengi kutendwa ama kutokea katika uongozi wa Rais Samia huku historia ikimdhihirisha kuwa Rais wa kwanza Mwanamke katika Taifa hili toka kuasisiwa kwakwe.

Pamoja na matarajio mengi ya watu kutoka kwake kuwa ni matarajio ya siasa safi na maendeleo ya watu, kama watanzania siku zote kiongozi hutazamwa kama mfano bora wa kuigwa na jamii katika mambo yote ikiwemo suala la maadili na uadilifu, huku mavazi na muonekano wa Kiongozi ukitarajiwa kuwa usiopotosha maadili ya jamii yetu.

Rais Samia ninaweza kusema wazi bila kificho kuwa amefanyika darasa kwa wanawake wa Tanzania na ulimwenguni kote katika kulinda utu na heshima ya mwanamke kwa kuvaa vizuri jambo linalothibitisha Uafrika na Utanzania wetu kama bara lenye kujali thamani ya mama na kama Taifa lenye kulinda utu wa mwanamke, huku mwanamke akitarajiwa kuwa mstari wa mbele katika kulinda utu na thamani yake.

Ninasema hivyo na kuwaasa wanawake wakitanzania kuendelea kulinda tunu hii njema kwa kuiga na kubadili mtindo wa mavazi usiofaa mbele ya macho ya jamii, maadili na tunu za taifa letu na kuvaa kwa heshima wakistiri miili yao.

Sote tutakubaliana kuwa katika ulimwengu huu wa maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia hali sio nzuri katika eneo hili la mavazi. Katika mitandao kijamii ndiko tunakoweza kuona zaidi sura zetu na kutazama sana maudhui tunayoweka. Inasikitisha sana kuona mwanamke wa Kiafrika na Mtanzania akiwa katika picha au video inayomuonesha kavalia mavazi yasiyo na stara(heshima), mavazi yanayomwonesha Shemu nyeti za mwili wake, huku akijua kuwa Dunia nzima inatazama, watoto wake na watoto, wana wa Afarika na Taifa letu wataona na kujifunza yasiyo adili kwao na Taifa letu. Ndio maana nasema hudhurieni darasa la mavazi kwa Rais Samia.

Rais mstaafu  wa awamu ya pili wa JMT Ally Hassani Mwinyi amewahi kusema

 _"Maisha ni hadithi tu hapa ulimwenguni ewe ndugu yangu  jitahidi uwe hadithi nzuri kwa wale watakao simuliwa habari yako"_

Wewe kama mwanamke baada yako, watoto wako watasimuliwa nini juu ya mavazi yako, wataona nini katika mitandao, watoto wenzao wataona nini juu ya mama wa rafiki zao, je watawacheka ,kuwazomea au kuwahurumia? Uchaguzi ni sasa na ni juu yako!

Ni wakati sasa tunaposhangilia mwanamke Mtanzania kuinuliwa katika nafasi za juu za uongozi, wanawake msisahau kuinuka katika suala la mavazi kwani sifa njema ya mwanamke ni stara ,ni kuvaa kwa heshima na kulinda thamani yake kama Dada, Mama, shangazi ama mke, na katika hao kama kiongozi wa familia na Taifa bora.

Sisemi kuwa mvae mavazi ya gharama kama Rais Samia HAPANA..!  Kila mja kwa uwezo alojaliwa na mwenyezi Mungu yapo mavazi mazuri ya heshima na stara yanapatikana kwa bei rahisi kabisa na yapo kila mahali.

Mwanamke mzuri siku zote si yule mwenye kuvalia nusu uchi ili atamaniwe na wanaume ama mwenye kila sifa mbaya katika jamii HAPANA!  Bali ni yule mwenye kujitunza  na kujiheshimu, mwenye kutunza thamani ya utu wake na zaidi kurithisha kizazi kinachokuja, kapu la maadili mema.

Mwisho niwaombee wanawake wote wa Taifa letu zuri la Tanzania, afya njema, uvumilivu , upendo kwa familia na watu wote ,uthubutu katika kazi na kujituma wakati wote katika ujenzi wa familia bora na Taifa letu.

Heko kwako Rais Samia kwa kuwa Rais Bora mwenye kufundisha kwa matendo yako, sifa njema ya mwanamke wa Kiafrika na Mwanamke wa Kitanzania. Hakika wewe ni mama Bora!

_Kwa maoni na mawasiliano zaidi juu ya makala zangu_

Simu: 0657221113/0758496706
Email: gregorypaul723@gmail.com

_DSM: Tanzania

No comments