TANZANIA INA WAFUNGWA NA MAHABUSU WA KISIASA

ASKOFU MWAMAKULA;
Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye ninamheshimu sana, Ndugu Gerson Msigwa, amekaririwa na Vyombo vya Habari nchini akisema kuwa Tanzania haina wafungwa wa kisiasa! Sasa nisikilizeni mimi niliye Askofu nikitoa maoni yangu tofauti na maoni ya Serikali kupitia kwa Gerson Msigwa. Kwanza kabisa, ninataka kuweka wazi kuwa Tanzania inao wafungwa na mahabusu wa kisiasa na hawajawahi kukosekana katika kila awamu ya uongozi, ingawa walizidi sana katika Awamu ya Tano

Mfungwa au mahabusu wa kisiasa ni mtu ye yote ambaye amekamatwa, akawekwa kizuizini na hata kuhukumiwa kifungo kwa sababu za kisiasa. Katika nchi kama Tanzania, Serikali hutumia maneno ya kificho yaani yasiyo ya moja kwa moja kama vile uchochezi, uhujumu uchumi, na hata utakatishaji fedha ili kuuhadaa umma na ulimwengu kuwa nchi haina wafungwa wa kisiasa! Mtu ye yote anayelengwa na kisha kukamatwa na kuwekwa mahabusu na hata kufungwa kwa mambo yafuatayo atachukuliwa kama mfungwa au mahabusu wa kisiasa: kuikosoa Serikali, kusaidia harakati za kisiasa, kuchapisha machapisho ya kisiasa, kufadhili shughuli za kisiasa, nk.

Makundi ambayo huongoza kutoa wafungwa wa kisiasa nchini Tanzania ni pamoja na wanasiasa, Waandishi wa Habari, wafanyabiashara, wanaharakati na hata viongozi wa dini. Kwa sababu kama zilizoelezwa hapo juu, wahusika hutafutiwa tuhuma au makosa mbalimbali ili kuuhadaa umma na ulimwengu ili wasijue kuwa wahusika wamelengwa kwa sababu za kisiasa.

Mheshimiwa Sugu, Mheshimiwa Lema, Mheshimiwa Mbowe, na viongozi kadhaa wa CHADEMA walihukumiwa kwenda jela kwa sababu za kisiasa. Tito Magoti, Erick Kabendera na watu wengine kadhaa walikaa mahabusu kwa muda mrefu kwa sababu zinazoingia katika fungu la wafungwa au mahabusu wa kisiasa. Mdude Nyagali Chadema anakabiliwa na mashtaka ambayo kimsingi yamechochewa na sababu za kisiasa.

Viongozi kadhaa pamoja na wafuasi wengi wa CHADEMA wako mahabusu hadi sasa kwa sababu za kisiasa. Moses Mwaifunga ambaye ameachiwa hivi karibuni alikuwa mahabusu au mfungwa wa kisiasa. Kiongozi wa ACT Wazalendo, Mheshimiwa Zitto Kabwe aliwahi kukabiliwa na mashtaka ya uchochezi ambayo kimsingi ni ya kisiasa!

No comments