RAIS SAMIA AMEWAHAKIKISHIA WAFANYAKAZI KUWA SERIKALI YA AWAMU YA SITA ITAJALI MASLAHI YA WAFANYABIASHARA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wafanyakazi wote kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi na kuboresha mazingira ya kazi ili waweze
kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Mhe. Rais Samia amesema hayo leo tarehe 01 Mei, 2021 katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani zilizofanyika kitaifa katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza na kuhudhuriwa na viongozi wakuu wakiwemo Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa
Majaliwa, Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Hussein Athman Kattanga, Mawaziri, viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na wafanyakazi wakiongozwa na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Bi. Tumaini Nyamhokya.
Mhe. Rais Samia amesema katika juhudi za kuboresha maslahi ya wafanyakazi Serikali
ya Awamu ya Sita imeamua kupunguza kodi ya mishahara kutoka asilimia 9 ya mwaka
2020/21 hadi asilimia 8 kuanzia mwaka 2021/22, ameitaka Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuharakisha mchakato wa kujadili, kufunga
na kuidhinisha mikataba ya hali bora ya wafanyakazi, ameielekeza mifuko ya hifadhi
ya jamii kuwalipa mafao yao wastaafu ambao wamesubiri muda mrefu kuanzia mwezi
huu na kulipa madeni ya watumishi.
Hatua nyingine ni kurejesha baadhi ya huduma za bima ya afya zilizokuwa zimeondolewa kufuatia marekebisho yaliyofanywa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya mwaka 2018, kuongeza umri wa watoto wategemezi wa bima ya afya kutoka
miaka 18 hadi 21 na kuangalia uvrezekano wa kugharamia matibabu kwa kundi la wastaafu bila kuzingatia kigezo cha miaka 10 ya uchangiaji, kuondoa tozo ya asilimia 6 ya kulinda thamani ya mkopo kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.
Aidha, amesema Serikali inakusudia kuwapandisha vyeo watumishi 85,521 (anto
wataigharimu shilingi Bilioni 119, kulipa malimbikizo ya mishahara yenye thamani ya shilingi Bilioni 60, kufanya mabadiliko ya miundo ya utumishi yatakayogharimu shilingi Bilioni 120 na kuajiri watumishi wapya 40,000 ambao wataigharimu shilingi Bilioni 239.
Mhe. Rais Samia amesema kwa kutambua kuwa wafanyakazi wa sekta binafsi hawajapandishwa mishahara kwa miaka 8 na wafanyakazi wa sekta ya umma hawajapandishwa mishahara kwa miaka 6, amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Vijana, Kazi na Wenye Ulemavu Mhe. Jenister Mhagama kufufua bodi za mishahara ili zifanyie kazi changamoto hiyo.
Kuhusu ombi la wafanyakazi kuongezewa mishahara, Mhe. Rais Samia amesema Serikali haitaweza kupandisha mishahara kwa sasa kutokana na changamoto za kushuka kwa ukuaji wa uchumi kutoka asilimia 6.9 hadi 1.7 kulikosababishwa na janga la ugonjwa wa Korona na hatua za Serikali kuleta nafuu kwa wananchi kwa kurekebisha mfumo wa viwango vya kodi kunakotarajiwa kupunguza mapato.
Amewahakikishia wafanyakazi wote nchini kuwa miradi yote ya kimkakati iliyoanzishwa katika Awamu ya Tano chini ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli itaendelezwa hasa ikizingatiwa kuwa imo katika mpango wa Taifa wa maendeleo wa 3
wa mwaka 2021-26 ikiwemo miradi inayotekelezwa katika Mkoa wa Mwanza ambayo
ni ujenzi wa daraja la Kigongo - Busisi, ujenzi na ukarabati wa meli katika Ziwa Victoria, ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege wa Mwanza na ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha Mwanza - Isaka.
Pia amesema Serikali itaendelea kuboresha huduma za elimu, maji na afya ikiwemo
hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Mwanza (Sekou Toure) hatua ambazo zitaendelea kulijenga Jiji la Mwanza kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wa Maziwa Makuu.
Rais wa TUCTA Bw. Tumaini Nyamhokya amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa
kuungana na wafanyakazi katika maadhimisho hayo na amemhakikishia kuwa wafanyakazi wote wanamuunga mkono na wapo tayari kutimiza wajibu wao kwa maslahi ya Taifa.
Mhe. Rais Samia amerejea Jijini Dodoma.
Post a Comment