RAIS SAMIA AMEKUTANA NA MKURUGENZI NATALIA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 11 Mei, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa (UNFPA) Dkt. Natalia Kanem, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo yao, Mhe. Rais Samia ameishukuru UNFPA kwa ushirikiano wake mzuri na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na ujauzito kwa mabinti wadogo, vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua, kukabiliana na ukatili wa kijinsia na
ukeketaji.
Mhe. Rais Samia amemhakikishia Dkt. Natalia kuwa atakuwa balozi mzuri wa kuhakikisha juhudi za kuwanusuru wanawake wanaojifungua wasipoteze maisha na kupiga vita mimba za utotoni na ameiomba UNFPA kuendelea kushirikiana na Tanzania ikiwemo kufadhili miradi ambayo inatekelezwa hapa nchini.
Kwa upande wake Dkt. Natalia amesema Umoja wa Mataifa wana matumaini makubwa na uongozi wa Mhe. Rais Samia na amemhakikishia kuwa UNFPA itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi na shughuli
mbalimbali shirika hilo.
Ameongeza kuwa kwa kutambua umasikini unaozikabili familia nyingi hasa vijijini UNFPA inatekeleza mkakati wa sifuri 3 ambapo kwanza inawasaidia wanawake wanaume kushirikiana kupanga familia zao vizuri ili kujenga familia imara na zenye furaha, pili ni kuhakikisha hakuna mwanamke anayepoteza maisha wakati wa
kujifungua kwa kuhakikisha wanawake wanajifungua katika vituo vyenye huduma,
mabinti wadogo hawabebi ujauzito wakiwa na umri mdogo na kukomesha ukeketaji, na tatu ni kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika Mhe. James Philip Duddridge Katika mazungumzo hayo, Mhe. Rais Samia amezikaribisha kampuni za Uingereza kuwekeza nchini Tanzania katika maeneo mbalimbali yenye fursa na ameelezea kufurahishwa na ujio wa Mhe. Duddridge ambao utafungua milango zaidi.
Mhe. Rais Samia amesema Serikali ya Awamu ya Sita ipo tayari wakati wote kuhakikisha uwekezaji huo unafanikiwa na amebainisha kuwa tayari imeanza kuchukua hatua za kuboresha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwemo
kuweka sawa masuala ya kikodi na vivutio vingine ili wawekezaji wengi zaidi wajitokeze.
Ameiomba Uingereza iendelee kuiunga mkono Tanzania katika juhudi zake za maendeleo na kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya na masuala ya mazingira Kwa upande wake Mhe. Duddridge amesema ana imani kubwa na uongozi wa Mhe. Rais Samia kuwa utaendeleza kazi nzuri iliyofanywa na mtangulizi wake Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na amemhakikishia kuwa Uingereza itaendelea
kushirikiana na Tanzania na kampuni za Uingereza zitaongeza uwekezaji hapa nchini.
Post a Comment