MISIKITI ITUMIKE KATIKA MASUALA YANAYOHUSU JAMII

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kwamba mbali ya ibada ni vyema misikiti ikatumiwa katika masuala yanayohusu jamii.
 
Alhaj Dk Mwinyi aliyasema hayo leo wakati akitoa nasaha zake katika ufunguzi wa Masjid Shifaa,  Mwembetanga, Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi, hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbali mbali wa dini na Serikali pamoja na waumini wa dini ya Kiislamu.
 
Alhaj Dk. Mwinyi ambaye mapema aliungana  wa Waumini wa dini ya Kiislamu katika Sala ya Ijumaa katika msikiti huo, alisema kuwa misikiti ina kazi zaidi ya ibada hivyo ni vyema Waumini wa dini ya Kiislamu wakaitumia kama alivyokuwa akifanya kiongozi wa Waislamu Bwana Mtume Muhammad (S.A.W) katika uhai wake.
 
Alisema kuwa katika jamii kuna matatizo mengi ambayo yanapaswa kujadiliwa na kufanyiwa kazi misikitini ikiwa ni pamoja na kuangalia utaratibu wa kuwasaidia wajane, wazee, watu wenye mahitaji maalum, kupambana na wizi, kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya pamoja na udhalilishaji ambayo yapo katika jamii.
 
Aliongeza kuwa matatizo kadhaa katika jamii yakiwemo wizi na matumizi ya dawa za kulevya na udhalilishaji jamii imekuwa ikivitegemea sana vyombo vya usalama peke yake katika kupambana na majanga hayo jambo ambalo iwapo misikiti ikitimiwa vyema inaweza kutoa msaada mkubwa.
 
Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa misikiti inaweza kutumiwa zaidi ya ibada ya sala na badala yake ikawa ndio sehemu ya mafunzo ya dini ya Kiislamu kwa kufundisha  darsa pamoja na mafunzo mengine ya dini hiyo.
 
Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Mwinyi amewataka Waumini wa dini ya Kiislamu kudumisha utamaduni wa matengenezo ya misikiti kwani mara baada ya kufunguliwa matengenezo huwa hayafanyiki na kusababisha kuanza kuharibika mapema.

No comments