AMKA NA BWANA LEO 29

KESHA LA ASUBUHI

JUMAMOSI, MEI, 29, 2021
SOMO: KUUNYENYEKEA UTUME

Wakiishika siri ya imani katika dhamiri safi.

 1 Timotheo 3: 9. 



Ninamtukuza Bwana asubuhi hii kwa amani ninayoifurahia. Kuna pumziko kamilifu kwa ajili yangu katika Bwana. Ninautumaini upendo wake. Kwa nini tusipumzike katika upendo wa Mungu, uhakikisho wa neno Lake? Yesu anasema nini? “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.” Ni jambo gani zuri zaidi ya ahadi hii? Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu. Kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.” (Mathayo 11:28—30). Basi njooni; hebu sisi tunaomwamini Yesu Kristo tusichelewe hata kidogo, bali njooni. 



Wale wanaojiangalia sana wao wenyewe, kana kwamba Bwana Yesu hamaanishi kabisa kile anachosema, wanaonesha kutomheshimu Mungu. Kwa kukaa mbali na Yesu, si kwamba matendo yetu yanasema, "Siamini kama Bwana Yesu anamaanisha anachokisema"? Huwatendei mema marafiki zako wa kibinadamu kwa namna hii ya mashaka na kutokuamini. Ikiwa watakuonesha heshima, ikiwa watakupatia ahadi, husemi, “Sina imani; siwezi kuiamini ahadi yako yoyote. Hii inanitia katika jaribu sana, hata hivyo siwezi kuliamini neno lako.” 



Kimsingi unamwambia Mungu haya yote katika matendo yako.... Daima umekuwa ukipata pumziko pale unapokuja, lakini unaanza kuhoji, kujiangalia mwenyewe, na kugugumia. Sasa acha haya yote. Iondoe hiyo nira ambayo umejitengenezea kwa ajili ya shingo lako ambayo inachubua sana, chukua nira ya Kristo, ambayo anatangaza kuwa ni laini, na mzigo wake ambao anakuambia ni mwepesi... 



Roho Mtakatifu ni Mfariji, Mfariji wako. Je, Roho Mtakatifu ameshindwa kutimiza sehemu yake ya kazi? Ikiwa ndivyo hivyo, basi hupaswi kulaumiwa. Lakini ahadi hii ni hakika na kweli. Unaposema kwamba huna imani kwa Mungu unamfanya Mungu kuwa mwongo na kuonesha kwamba huna imani na kazi ya Roho Mtakatifu, ambaye daima yupo tayari kutusaidia udhaifu wetu. 



Daima anasubiri mlangoni kwako, daima anabisha ili akaribishwe. Mkaribishe aingie. Unachopaswa kufanya ni kusalimisha nia yako kwa mapenzi ya Bwana. Unahitaji ahadi, lakini unapaswa kuwa na ujasiri mkamilifu kwa Yule ambaye ameitoa ahadi hiyo. Sema hivi: “Mimi ni wa Bwana. Ninaamini.” Ondoa kila mashaka kutoka moyoni. Mwamini Mungu. Anakupenda. Kamwe, usiruhusu mashaka ndani yako au kutomwamini.



—Manuscript 80, Mei 29, 1893,, shajara

No comments